BALOZI wa Tanzania Ujerumani, Hassan Iddi Mwamweta amesema Tanzania imedhamiria kupanua wigo wa biashara ya matunda na mboga katika soko la dunia ili kuinua uchumi wa wakulima nchini.
Balozi Mwameta ameyasema hayo kwenye banda la Tanzania katika maonesho ya Fruit Logistica 2025 yanayofanyika jijini Berlin.
Amepongeza juhudi zinazofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kilimo cha Matunda na Mbogamboga (TAHA) na sekta binafsi, akisema ni hatua muhimu kuyafikisha mazao ya kilimo yanayozalishwa nchini katika masoko ya kimataifa.
“Kulipata Soko la Ulaya si kazi rahisi, tunahitaji mikakati madhubuti na ushirikiano imara wa sekta ya umma na sekta binafsi,” amesisitiza Balozi Mwamweta.
Amesema wafanyabiashara wa Tanzania wanatakiwa kuwa na juhudi kutengeneza fursa za masoko, kuanzisha ushirikiano na kujifunza kutoka kwa wadau wa kimataifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Irene Mlola, amesema kuna umuhimu kwa Tanzania kushiriki katika maonesho ya aina hiyo kwa kuwa ni sehemu ya majukwaa yanayosaidia kusogeza mbele ajenda ya kilimo cha Tanzania, kitaifa na kimataifa.
Irene, amefafanua kuwa miongoni mwa matokeo yanayoweza kupatikana kwenye ushiriki huo ni ubia mpya wa biashara kati ya wauzaji bidhaa kutoka Tanzania na wanunuzi wa kimataifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED