Serikali yaweka mkazo zaidi sekta ya mazao ya nyuki

By Ida Mushi , Nipashe
Published at 06:49 PM Feb 19 2026
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Chande.
Picha:Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Chande.

Serikali imeweka mkazo mpya katika sekta ya mazao ya nyuki, ikilenga kuongeza uzalishaji wa asali kwa ajili ya soko la nje na kukuza uchumi wa taifa.

Hayo yamesemwa mjini Morogoro na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Chande, wakati akizungumza na makamanda na maafisa wa TFS ambapo akawahimiza kuwa wabunifu ikibidi kuanzisha tiba itokanayo na nyuki na mazao yake na kliniki maalum itakayovuta wageni kutoka ndani na nje ya nchi na kuingiza pato la nchi.

Chande amesema pamoja na mafanikio yaliyopo, bado kuna fursa kubwa katika bidhaa nyingine za nyuki kama sumu na chavua, akisisitiza kuwa tafiti na ubunifu ni muhimu ili kufikia masoko ya kimataifa.

Ameongeza kuwa jamii zinazozunguka hifadhi zinapaswa kuendelea kuelimishwa kuhusu ufugaji wa kisasa wa nyuki, ili kuongeza uzalishaji na kuboresha maisha yao.

Amewataka viongozi wa TFS kuwekeza katika elimu kwa watumishi wao, akisema hatua hiyo itaimarisha ufanisi na uaminifu kazini.

Naye Kamishna wa Uhifadhi wa TFS Prof.Dos santos Silayo amesema mkutano huo ni sehemu ya kuimarisha nidhamu na uwezo wa askari huku Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bernard Marceline, akipongeza utendaji kazi wa TFS na kuutaja kuwa wa mfano Serikalini