Serikali yakanusha upungufu wa mafuta

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 01:06 PM Feb 20 2026
Kituo cha mafuta.
Picha:Mpigapicha Wetu
Kituo cha mafuta.

Licha ya malalamiko ya wananchi kuhusu uhaba wa petroli katika baadhi ya vituo vya mafuta visiwani, Serikali ya Zanzibar imesisitiza kuwa hakuna upungufu wa mafuta na kwamba akiba iliyopo inatosha kukidhi mahitaji ya sasa.

Akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Paje, Jaku Hashim Ayoub, katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kilichofanyika Chukwani, Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Nadil Abdullatif, amesema kwa sasa kuna zaidi ya lita milioni tatu za petroli na lita milioni saba za dizeli zilizohifadhiwa Zanzibar.

Ameeleza kuwa changamoto iliyojitokeza hivi karibuni ilisababishwa na hitilafu ya kiufundi katika meli iliyokuwa imepangwa kuleta shehena ya mafuta, hali iliyopelekea kuchelewa kwa takribani siku mbili.

“Katika kipindi cha miaka sita ya uongozi wa Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi, hatujawahi kushuhudia hali kama hii. Ilikuwa ni tukio la kibinadamu tu na tayari tumelidhibiti,” amesema Waziri Nadil.

Ameongeza kuwa Serikali ilichukua hatua za haraka kuagiza meli nyingine kutoka Mombasa, nchini Kenya, na kwamba tangu juzi meli tatu zimewasili na kuanza kushusha mafuta.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliozungumza na Nipashe Digital  wameeleza kuwa bado kuna changamoto katika baadhi ya vituo vya mafuta, huku vingine vikifungwa kutokana na kukosa mafuta na vile vinavyotoa huduma vikishuhudia misururu mirefu ya magari.