SERIKALI ya Zanzibar imesema imejipanga kuimarisha huduma za upatikanaji wa umeme vijijini ambazo zitawawezesha wananchi kuacha kutumia kuni na mkaa ambayo ni tishio kwa uharibifu wa mazingira.
Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Shaibu Hassan Kaduwara, alisema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja katika ziara ya kuzipatia ufumbuzi changamoto za upatikanaji wa umeme na pamoja na kuongeza kampeni za kuacha kutumia kuni na mkaa.
Alisema katika mwaka wa fedha 2024-2025 Wizara ya Maji, Nishati na Madini, imejipanga kuongeza upatikanaji wa huduma za nishati ya umeme hadi vijijini ikiwamo kujenga laini nyingine mpya za umeme.
Alisema serikali imejipanga kuleta megawatti 220 na kuweka waya mpya kutoka Tanzania Bara huko Ras Kilomoni kutokana na waya unaotumika sasa kuwa na uwezo wa megawatti 132 KV.
Alisema umeme huo utakuwa na uwezo mkubwa kwa matumizi ya shughuli nyingi ikiwamo za maendeleo katika miradi ya viwanda na matumizi ya hoteli za kitalii.
Kaduwara alisema kwa upande wa wamiliki wa hoteli za kitalii wamekuwa wakipokea malalamiko makubwa ya kuwapo kwa umeme mdogo usiotosheleza matumizi ya hoteli hizo na kuibuka tatizo la kukatika mara kwa mara.
Aidha, aliwataka wanawake kujipanga zaidi kuingia katika mageuzi yaliopo sasa ya matumizi ya nishati asilia ya gesi na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.
Alisema hivi sasa maeneo mengi ya Mkoa wa Kaskazini Unguja pamoja na Pemba kumejitokeza tatizo la athari za mazingira yanayotokana na wananchi kukata miti kwa matumizi ya kuni na mkaa.
Alisema kwa upande wa Pemba kumejitokeza ukataji mkubwa wa mikoko ambayo ndiyo inayolinda hifadhi ya bahari na mabadiliko ya tabia nchi na matokeo yake kuwapo kwa athari kubwa za kasi ya maji kuja juu.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais anayeshughulikia Mazingira, Harusi Said Suleiman, alisema jamii hasa wanawake wameanza kuhamasika kuelekea matumizi ya gesi asilia sambamba na serikali kuweka mazingira mazuri ikiwamo kushusha kodi ya vifaa vya gesi asilia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED