Punda, mbwa waondolewa orodha wanyama wanaoliwa

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 07:25 AM Sep 30 2024
Mbwa na punda.
Picha:Mtandao
Mbwa na punda.

WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imefanya maboresho ya kanuni kwa kuwaondoa punda na mbwa katika orodha ya wanyama wanaotakiwa kuchinjwa na kufanywa kitoweo.

Naibu Mkurugenzi wa Haki za Wanyama na Ustawi wa Wanyama, Dk. Annette Kitambi, alisema hayo juzi wakati wa warsha ya wadau iliyolenga uwasilishaji wa tathimini ya ustawi wa wanyama.

Alisema marekebisho ya kanuni hiyo yatasaidia kumlinda mnyama punda ambaye katika baadhi ya mikoa imekuwa ikimchinja mnyama huyo na kufanywa kitoweo, jambo ambalo linahatarisha kutoweka.

Dk. Kitambi alisema hatua nyingine zinazochukuliwa na serikali ni kufanya marekebisho kwenye mitaala ya mafunzo, ili baadhi ya wanyama akiwamo punda waweze kutajwa vizuri na hivyo wasiweze kupotea nchini.

"Katika kuhakikisha punda wanakuwa wengi nchini, tumeona kuna umuhimu wa kufanya utafiti wa uzalianaji wa punda maana inawezekana tatizo la punda kutozaliana kwa wingi linazababishwa na matunzo duni anayopewa," alisema. 

Dk.Kitambi alisema pia serikali imekuwa ikitoa elimu ya ustawi wa mnyama punda kwenye minada, luninga na redio, uteuzi wa wakaguzi wa masuala ya ustawi wa wanyama katika mamlaka za serikali za nitaa na uteuzi wa bodi ya kumshauri waziri masuala ya ustawi wa wanyama nchini. 

Daktari wa mifugo kutoka sekta binafsi, Dk.Bedan Masuruli, akiwasilisha ripoti ya tathimini ya hali mnyama punda, alisema licha ya katazo la serikali lililotolewa 2021 lakini bado biashara ya mnyama huyo inaendelea kufanyika hapa nchini. 

Dk. Masuruli alisema hivi sasa punda wengi kutoka mikoa mbalimbali wanasafirishwa kupelekwa Mkoa wa Geita lakini bado haijafahamika wakifikishwa katika mkoa huo wanapelekwa wapi.

Alisema hata biashara ya ngozi ya punda bado inafanyika kwa kasi sambamba na kusafirishwa kutoka Tanzania Kwenda Kenya.

Alisema kuna haja kwa Serikali ya Tanzania ishirikiane na Serikali ya Kenya katika kudhibiti biashara ya punda.

Mkurugenzi wa Shirika la Inades Formation Tanzania (IFTz), Mbarwa Kivuyo, alisema shirika hilo kwa kushirikiana na Brooker East Africa wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha haki na ustawi wa mnyama punda analindwa.