Nyuki kuwatimua tembo kwenye makazi

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 10:07 AM Jan 03 2025
Nyuki.
Picha: Mtandao
Nyuki.

KIJIJI cha Nyuki Co.Limited Halmashauri ya Manispaa ya Singida kimetangaza mkakati wake kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kudhibiti tembo kuvamia makazi ya wananchi na kuharibu mali kwa kutumia nyuki.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kijiji hicho, Phillemon Kiemi akizungumza juzi na waandishi wa habari, alisema hatua hiyo inatokana na usumbufu wanaopata wakazi wa Mkoa wa Singida kwa kuvamiwa na tembo kwenye makazi yao  mara kwa mara. 

Kemi, alisema kijiji chao kinachojishughulisha na ufugaji nyuki, mwaka huu kimekuja na mbinu za kisasa kuwadhibiti wanyama hao. 

Alisema mapito ya tembo kwenye wilaya za mkoa huo zinazopata usumbufu wa wanyama hao, yataainishwa kisha kuweka mitego ya mizinga ya nyuki ambayo itatumika kuwafukuza kwenye makazi. 

"Kutumia wataalam wabobezi wa kijiji cha nyuki, tutatumia mbinu za kukabiliana na tembo hao kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na utalii," alisema. 

 Kiemi alitaja mikakati mingine ambayo wamepanga kufanya kwa mwaka huu kuwa ni kufungua ranchi ya ufugaji wa malkia wa nyuki.

Alisema lengo ni kusaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa nyuki  ambao kwa sasa unalalamikiwa na wafugaji wa nyuki nchini. 

Alisema mwaka huu wamepanga kutoa mafunzo kwa watu 10,000 kutoka vijiji vyote vya Mkoa wa Singida namna ya ufugaji nyuki na kuwapa mzinga  kila mmoja ili waanzishe mradi huo. 

Kazi nyingine zitakazofanyika ni kufungua viwanda vya kuzalisha mvinyo wa asali, kujenga hoteli na viwanja vya mpira ili timu kubwa nchini zitakapowasili Singida zifikie kijini kwao kufanya utalii na kupata huduma ya malazi. 

Kumekuwa na mfululizo wa matukio ya tembo kuvamia makazi ya watu na kubomoa nyumba katika Mkoa wa Singida. 

 Novemba 10, mwaka jana  tembo zaidi ya 56 walivamia Kijiji  cha Mkiwa wilayani Ikungi,  kuvunja nyumba nane na kula vyakula. 

Kufuatia tukio hilo, wakazi wa Kijiji hicho walifunga barabara kuu ya Dodoma-Singida na kumlazimu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Pindi Chana kufika  na kuagiza askari wa TAWA kuweka kambi kuwadhibiti wanyama hao. 

Kwa Mkoa wa Singida wilaya nyingine zinazokabiliwa na tatizo la tembo hao ni Manyoni, Singida na Halmashauri ya Itigi.