KATIBU Tawala Mkoa wa Njombe, Judica Omari, amesema kuna upungufu kwenye ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, kwamba kati ya makadirio ya Sh. bilioni tano zimekusanywa Sh. bilioni nne.
Aliyasema hayo katika kikao cha Baraza la Madiwani cha kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kilichofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.
Alisema kuwa upungufu huo umeonekana kwenye ushuru na kodi ya huduma ambapo asilimia 30 ya mapato hadi sasa haijakusanywa ambayo ni sawa na Sh. bilioni moja.
“Kwenye usimamizi wa mapato kwenye halmashauri bado kuna changamoto, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe mpaka sasa hadi Mei mwishoni imefikia asilimia 70 ya makusanyo yaliyopangwa kwa mwaka huu 2023/24 kiwango bado kiko chini,” alisema Omari.
Pia aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kwa maamuzi ya kuhamia ofisi ya makao makuu baada ya jengo lao kukamilika na kwamba kwa kufanya hivyo itasaidia kutoa huduma kwa haraka kwa wananchi.
Mkurugenzi wa Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Christopher Sanga, alisema halmashauri hiyo inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa watumishi katika kada mbalimbali.
Alisema halmashauri ilikuwa na hoja 12 sawa na asilimia 41.4 ambazo zimehakikiwa na mkaguzi na kufungwa, hoja 17 sawa na asilimia 58.6 zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali Mkoa wa Njombe, Willy Ondule, alishauri kufutwa kwa hoja za muda mrefu pamoja na kuacha kuzalisha hoja ambazo siyo za msingi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED