Nchemba aagiza KNCU kuuza mali zake kufidia deni

By Mary Mosha , Nipashe
Published at 04:30 PM Feb 20 2026
Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba.

Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba, ameiagiza Kilimanjaro Native Cooperative Union (KNCU) kuuza moja ya mali zake ili kufidia deni la zaidi ya Sh milioni 400 linalodaiwa na Chama cha Ushirika cha Msingi cha Mwika Kinyamvuo.

Agizo hilo amelitoa Februari 20, 2026 katika kijiji cha Chekereni, wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro Region, baada ya kupokea malalamiko ya wanachama waliouza kahawa yao kupitia KNCU mwaka 2023 lakini hadi sasa wamelipwa Sh milioni 90 pekee.

Akizungumza mbele ya wananchi, Dk. Nchemba amesema kuchelewa kulipa wakulima kunadhoofisha imani ya wananchi kwa vyama vya ushirika na Serikali.

“Ninyi msiolipa wananchi ndio mnapelekea wananchi kupoteza imani na Serikali yao. Haiwezekani jambo moja likachukua mwaka wa kwanza, wa pili, wa tatu na wa nne huku watu wanalia,” amesema.

Amesisitiza kuwa KNCU inamiliki mali zinazoweza kuuzwa ili kumaliza deni hilo mara moja badala ya kuendelea kuwalipa wakulima kwa awamu.

“Mlichukua kahawa zao tangu mwaka 2023 halafu mnataka kuwalipa kwa awamu. Ziuzwe hata mali ili wananchi walipwe fedha zao. Sitaki kusikia mambo ya kulipa mwakani,” amesisitiza.

Aidha, Waziri Mkuu amemwagiza Msajili wa Vyama vya Ushirika ngazi ya mkoa kushirikiana na uongozi wa KNCU kubaini mali itakayouzwa ili fedha zipatikane haraka na deni lote kulipwa.

Pia ameagiza bodi ya chama hicho kukutana ifikapo Jumatano ya wiki ijayo na kuwasilisha majibu rasmi ya utekelezaji wa maagizo hayo, akionya kuwa hatua kali zitachukuliwa iwapo hakutakuwa na utekelezaji.