OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) zinatarajia kuanza utafiti wa tatu kuangalia hali ya upatikanaji nishati kwa Tanzania Bara mwaka 2024.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk. Albina Chuwa, alisema hayo mjini hapa wakati akizungumza na wadadisi 110 waliokuwa wanafundishwa namna ya kufanya utafiti huo kutoka kwa wataalamu mbalimbali wakiwamo wa kutoka Wizara ya Nishati, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na NBS.
Dk. Chuwa alisema utafiti huo utazifikia kaya 10,500 za Tanzania Bara za mijini na vijijini pamoja na kuangalia matumizi ya nishati ya kupikia.
"Utafiti huu ni muhimu sana katika kutekeleza Maendeleo Endelevu ya Dunia ya mwaka 2030, Dira ya Taifa ya 2025 inayomalizika na ambayo haiwezi kumalizika bila kuwa na taarifa sahihi na ile ya 2025 hadi 2050, " alisema.
Dk. Chuwa alisema kuwa katika Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2002, hali ya wananchi kutumia nishati safi ilikuwa ndogo sana na alibaini ilikuwa asilimia moja pekee, tena kwa wananchi hasa wanaoishi katika majiji.
Alisema hata Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere katika miaka 63 iliyopita wakati nchi ikipata Uhuru, aliamini na kutoa umuhimu kwenye takwimu katika kupanga mipango ya maendeleo ya nchi, na ndivyo alivyowaridhisha marais waliomfuata
Kamishna wa Sensa na Spika mstaafu, Anne Makinda, alisema serikali imeendelea kutambua umuhimu wa sekta ya nishati katika kukuza uchumi wa nchi kwa kutekeleza mipango na programu mbalimbali za maendeleo kwa kuhakikisha umeme wa kutosha unakuwapo na kusaidia kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati kama reli ya kisasa ya SGR na kuzidi kuvutia wawekezaji katika uzalishaji wa bidhaa na huduma na kuimarisha uchumi na maisha ya wananchi.
"Mwekezaji hawezi kwenda kwenye maeneo hayana umeme wa uhakika kwa mujibu wa matokeo ya Utafiti, Hali ya upatikanaji wa Nishati Tanzania bara kwa mwaka 2019 uliofanywa na NBS kwa kushirikiana na REA ilionesha upatikanaji wa Nishati ulikuwa ni kwa asilimia78.5, mjini ulikuwa asilimia 99.6 na vijijini," alisema Makinda.
Kadhalika utekelezaji wa mpango kabambe wa kupeleka umeme vijijini umewezesha jumla ya vijiji 12,240 kati ya 12,318 vya Tanzania Bara, kufikiwa na umeme hadi kufikia Novemba, mwaka huu na wa bei nafuu na wa kuaminika na nguvu zaidi imeelekezwa kwenye vitongoji.
Kamishna huyo wa Sensa alisema usambazaji wa umeme vijijini utaharakisha utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia ambao umelenga ifikapo 2034 asilimia 80 ya wananchi wawe wanatuma nishati hiyo na kwenda sambamba na jitihada za serikali za kupambana na uharibifu wa mazingira unaotokana na matumizi ya nishati za kupikia zitokanazo na kuni na mkaa.
Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi kutoka NBS, Daniel Masolwa, alisema utafiti huo utafanyika ndani ya siku 30 na kuomba wananchi watakaofikiwa kutoa ushirikiano.
Mwakilishi wa REA mhandisi, Salma Bakari alisema utafiti huu ni wa tatu kufanyika kwa kushirikiana na NBS ukitatajiwa kuleta matokeo chanya kwenye kufahamu uhalisia wa mahitaji na kuyafanyia kazi.
Alisema tangu kuanzishwa kwa REA mwaka 2007 wameweza kutekeleza miradi 428 ilipofika Juni mwaka huu, ikiwamo inayohusika na Gridi ya Taifa na nje ya Gridi Taifa na kwamba wameendelea kupambana kufikisha nishati safi na bora vijijini na kuhimiza wadadisi kujali shughuli hiyo iliyo mbele ya utafiti kwani matokeo yake yanategemewa sana katika maendeleo ya nchi na mahusiano na wafadhili mbalimbali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED