Msalala yapanga bajeti Sh. bilioni 47.8

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 01:47 PM Feb 23 2026
Halmashauri ya Msalala kukusanya na kutumia Sh.bilioni 47.8 mwaka 2026/2027.
Picha: Mpigapicha Wetu
Halmashauri ya Msalala kukusanya na kutumia Sh.bilioni 47.8 mwaka 2026/2027.

Halmashauri ya Wilaya ya Msalala imepanga kukusanya na kutumia jumla ya Sh bilioni 47.8 katika mwaka wa fedha 2026/2027, huku ikielekeza nguvu kubwa katika kukamilisha miradi ya maendeleo iliyoibuliwa na wananchi, hususan katika sekta za elimu, afya na utawala.

Akizungumza katika Mkutano Maalumu wa Baraza la Madiwani wa kujadili rasimu ya mpango na bajeti hiyo, Kaimu Mkuu wa Idara ya Mipango na Uratibu, Thobias Likiliwike, amesema kati ya fedha hizo, Sh bilioni 9.5 zinatarajiwa kutoka kwenye mapato ya ndani, ikiwa ni ongezeko la Sh milioni 800 kutoka bajeti ya mwaka 2025/2026 ya Sh bilioni 8.758, sawa na ongezeko la asilimia 9.1.

Amefafanua kuwa Serikali Kuu itachangia Sh bilioni 4.6 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, Sh bilioni 1.6 kwa matumizi mengineyo, Sh bilioni 4.5 kutoka kwa wafadhili wa miradi ya maendeleo, pamoja na Sh bilioni 25.6 za ruzuku ya mishahara. Aidha, kiasi cha Sh bilioni 1.88 kinatarajiwa kupatikana kupitia fedha za uwajibikaji wa makampuni kwa jamii (CSR).

Likiliwike amewataka madiwani kushiriki kikamilifu katika kusimamia na kuhamasisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kufanikisha utekelezaji wa bajeti hiyo. Alisema halmashauri pia imepanga kutenga fedha kwa ajili ya kulipa madeni ya wazabuni na watumishi, pamoja na kuendeleza miradi ya kimkakati ya kuongeza mapato, ikiwemo soko la madini la Bugarama.

Katika kuimarisha ustawi wa jamii, halmashauri imepanga kutekeleza afua za lishe kwa kutenga Sh 1,000 kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano. Pia, asilimia 60 ya mapato ya ndani yatatengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, sambamba na kuwawezesha wajasiriamali vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, pamoja na kuimarisha usimamizi wa rasilimali na mazingira.

Diwani wa Kata ya Ikinda, Matrida Musoma, amesema madiwani watahakikisha wanasimamia ipasavyo vyanzo vya mapato vilivyopo na kuibua vipya ili kufanikisha utekelezaji wa miradi mingi inayosubiri kukamilishwa.

Kwa upande wake, Diwani wa Busangi, Vicent Magembe, amewataka wataalamu wa halmashauri kusimamia kwa karibu miradi inayoendelea kutekelezwa ili ikamilike kwa viwango vinavyokubalika, akisisitiza kuwa fedha za umma lazima zitumike kwa uadilifu na kuakisi mahitaji halisi ya wananchi.