Uamuzi wa serikali kuja na mizani za kidijitali ili kudhibiti unyonyaji wa wakulima katika mazao, kumegeuka kuwa suluhisho la kudumu la kupunguza malalamiko, ubadhirifu.
Hatua hiyo imetajwa kuongeza imani ya wakulima kwenye sekta ya ushirika, kwamba matumizi hayo yamesababisha wakulima kupata taarifa sahihi ya kila hatua ya mauzo na kiasi cha fedha wanachostahili kulipwa.
Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dk. Benson Ndiege, ameeleza hayo jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha sita cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA).
Amesema mifumo hiyo ya kidijitali imeongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji, kuboresha utendaji, kuchochea mabadiliko ya kiuchumi, kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi na kuongeza udhibiti katika usimamizi.
Amesema hadi kufikia Juni 30 mwaka jana vyama 4,634 vilikuwa vinatumia mizani ya kidijitali yenye thamani ya Sh. bilioni 15.16.
“Tume kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao, imetengeneza mfumo wa kidijitali wa usimamizi wa vyama vya ushirika. Mfumo huu umeleta mabadiliko chanya katika uendeshaji na usimamizi wa vyama vya ushirika nchini.
…Ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa, kupunguza udurufu wa mifumo na gharama za uendeshaji, mfumo wa vyama vya ushirika umejiunga na Mfumo Mkuu wa Serikali wa Ubadilishanaji Taarifa (GovESB), ambapo hadi sasa mifumo tisa ya taasisi za serikali imeunganishwa.” amesema.
Dk. Ndiege amesema mifumo ya kidijitali inaendelea kusambazwa katika vyama vya ushirika vya kilimo, ufugaji, uvuvi, uchimbaji madini na vinginevyo.
Hata hivyo, taarifa ya takwimu za vyama vya ushirika ya Julai 2024 – Juni 2025 inaonesha kuwa hadi mwaka 2025, vyama vilivyokuwa vimesajiliwa ni 7,984 wakati mwaka 2024 vilikuwa 7,604.
Katika msimu wa kilimo wa mwaka 2024/2025, vyama vya ushirika viliuza tani 2,237,372.47 za mazao mbalimbali yenye thamani ya Sh.trilioni.4.28.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU), Julius Mollel, amesema jitihada hizo zimesaidia kupunguza malalamiko na ubadhirifu na kuongeza imani kwenye sekta ya ushirika.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED