Mhandisi Mramba: Huduma ya umeme imeimarika

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 11:45 AM Jul 10 2024
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Felchesmi Mramba kushoto akizungumzia hali ya umeme nchini.
Picha: Maulid Mmbaga.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Felchesmi Mramba kushoto akizungumzia hali ya umeme nchini.

KATIBU Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema ubora wa huduma ya umeme umeimarika hivyo kukatika na mgao hakuna na wanaendelea kuboresha, hivyo ni wajibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kusimamia.

Akizungumza leo mkoani Dar es Salaam katika maonyesho ya 48 ya biashara ya kimataifa Sabadaba, amesema huduma za umeme ni moja ya sehemu ambayo inadhibitiwa na EWURA ambayo ameonyesha kufurahishwa na utendaji wake.

Amesema EWURA wameweza upatikanaji wa huduma yenyewe, bei na ubora wake, akieleza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye bei ya chini zaidi ya huduma ya umeme ikilinghangishwa na mataifa jirani.

“Hatusemi kwamba ubora sasa umefikia mahali ambako hakuna shida hapana, lakini angalau huduma hiyo iko katika kiwango cha kuridhisha. Na tunaendelea kuboresha, kwahiyo ni wajibu wa EWURA kudhibiti na kusimamia,” amesema Mhandisi Mramba.

Ameongeza kuwa katika maeneo ya Gesi asilia mamlaka hiyo imesaidia sana na inaendelea kutoa leseni kwa wa wanaojenga vituo vya (CAG) kwaajili ya magari na bajaji zinazotumia mfumo wa Gasi, pamoja na vya mafuta.

1

Aidha, alieleza kuwa jukumu linguine la EWURA ni kuhakikisha huduma inayotolewa na vituo husima zinakidhi mahitaji ya jamii.

“Nasisi kama wizara wajibu wetu ni kuhakikisha EWURA anafanya kazi yake kwa mujibu wa sharia na sera zilizoko, lakini pia tunamuwezesha kutekeleza majukumu yake katika mazingirta yanayokubalika ndani ya sekta.

“Pia tunataka kuendelea kuwatia moyo watanzania, ziko huduma nyingi zinazotolewa na mamlaka hii zikiwemo za kiushauri, kupokea malalamiko na ni wajibu wa EWURA kuyasikiliza na kuyafanyia kazi, pia tunampongeza kwa kazi nzuri inayoifanya,” amesema Mhandisi Mramba.

Naye, Mkurugenzi wa EWURA, James Andilile amesema wameingia mkataba na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa lengo la kusimamia utendaji kazi wao ili kuboresha upatikanaji wa nishati hiyo, na kwamba serikali inafanya uwekezaji mkubwa katika kuhakikisha sekta hiyo inaimarika.

2