KAMPUNI ya M/S Brodosplit JSC ya Nchini Croatia kwa kushirikiana na Kampuni ya kizalendo ya Dar es Salaam Merchant Group (DMG) wamekabidhiwa rasmi meli kongwe ya MV. Liemba ambayo ni maalumu kwa abiria na mizigo iliyopo mkoani Kigoma (Ziwa Tanganyika) ili waanze mara moja ukarabati wa viwango ambao utachukua takribani miaka miwili.
Akizungumza jana mkoani Kigoma mara baada ya makabidhiano, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Dar es Salaam Merchant Group (DMG), Rayton Kwembe amesema kuwa ukarabati wa meli hiyo kongwe ya abiria na mizigo ya MV. Liemba utatumia gharama ya shilingi bilioni 33 na amesisitiza watajitahidi kufanya kazi kwa wakati na weredi wakishirikiana na mkandarasi mkuu ambaye ni Kampouni ya M/S Brodosplit JSC ili kwenda sambamba na muda uliopangwa kwenye mkataba.
“Tunaahidi ukarabati uliotukuka na wenye viwango ambapo kwenye utekelezaji huu tunafanya kwa ushirikiano na Kampuni ya M/S Brodosplit JSC ya Nchini Croatia ambao ndiyo wakandarasi wakuu kwenye mradi huu wenye gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 33.”
Kwembe aliongeza: “Tunaishukuru sana serikali yetu ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuamini na tunaiahidi Serikali kuwa kamwe hatutawaangusha katika utekelezaji wa mradi huu.”
Alisisitiza kwa kusema, “Tutajitaidi kwa hali na mali kuhakikisha kuwa miradi huu wa ukarabati tunaufanya kwa muda muafaka ili meli hii ambayo ni maalumu kwa usafirishaji wa mizigo na abiria iendelee kufungua fursa nyingi za ajira binafsi na kupunguza gharama za usafirishaji sambamba na kuongeza tija katika shughuli za biashara na hivyo kuwafanya wananchi kunufaika.”
Mkurugenzi huyo wa DMG alidokeza kuwa kampuni yao ina uzoefu wa muda mrefu na utaalam wa kushiriki katika miradi mikubwa inayohusisha matengenezo ya meli na uundaji kwa ujumla kutoka hatua ya awali mpaka kukamilika.
Alibainisha: “Lakini pia Kampuni yetu ya DMG ipo katika mahusiano mazuri na taasisi za fedha ambapo mahusiano haya yanatusaidia kupata fedha stahiki kwa wakati pale zinapoitajika ili kusaidia miradi yetu kwenda na muda ulipangwa."
Alisisitiza: "Ili kutekeleza vyema miradi ya ujenzi wa meli na matengenezo yake, DMG ilianzisha Idara ya kushughulikia mambo hayo mwanzoni mwaka 2017 kwa nia ya kutatua changamoto zinazoikabili Sekta hii iliyo katika uchumi wa bluu kwa kuleta maendeleo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Salum Kalli amewataka wakandalasi wa mradi huo wa ukarabati wa meli hiyo kukamilisha kazi waliyopewa kwa wakati kama ambavyo imebainishwa kwenye mkataba wa makubaliano.
“Cha msingi ni kuendana na matakwa ya mkataba,. hakika ilikuwa ni ndoto lakini sasa imetimia, watu wa Kigoma na Watanzania kwa ujumla wana furaha kusikia habari hii kuwa sasa ukarabati wa meli hii unaanza rasmi,” alisema DC Kalli.
Allen Mtembelo, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huduma za Meli (Mscl), amesema: “Wakandarasi tayali wapo site na wapo tayari kuanza mradi huu wa ukarabati wa Mv Liemba.”
Serikali iliamua kuwekeza katika ukarabati wa meli hiyo kutokana na uimara wake na kuokoa gharama ya kujenga au kutengeneza meli mpya.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya meli hiyo Meneja wa Mradi huo Mhandisi Luteni Kanali Elias John Kivala amesema: “Kwa niaba ya serikali, tunawaomba wakamilishe mradi huu kwa muda muafaka, na tunawaomba wafanye fast track (haraka zaidi), kama serikali tunawaahidi kuwapa ruhusa ya kufanya kazi kwa masaa 24.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED