Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita ametoa wito kwa kampuni za sukari na serikali huhakikisha wakulima wa miwa wanapata stahiki ya jasho lao kwa wakati, bei nzuri na usalama wa mashamba yao.
Akiwa katika Jimbo la Mikumi juzi Septemba 28, 2024, Mchinjita alisema kuwa wakulima wamemlalamikia matatizo mbalimbali wanayokumbana nayo na kumwomba apaze sauti ili serikali na wanunuzi (viwanda ) visikie kilio chao.
Matatizo hayo ni pamoja na kuchelewa kwa malipo ya miwa baada ya kupokelewa viwandani ambapo malipo hayo huchukuwa mpaka siku 45 baada ya kupokelewa, kutoshirikishwa upangaji wa bei na kutotabirika kwa bei ambapo Mchinjita alisema mwaka juzi tani moja ya miwa ilinunuliwa kwa 90,000 lakini msimu huu Tani Moja ni 70,000, changamoto nyengine ni kuunguliwa kwa moto katika mashamba ya miwa.
"Katika Nchi ambayo kila mwaka inakua na uhaba wa sukari lakini wakulima wa sukari yenyewe hawathaminiwi, bei ya miwa ni ndogo lakini bei ya sukari ni kubwa." alisema Mchinjita.
Aidha kiongozi huyo alisema; "Kilimo kimeajiri takribani 70% ya Watanzania wote, kinachangia asilimia 26 ya Pato la Taifa. Lakini wakulima hawathaminiwi.Huwezi kuendeleza nchi hii bila kuendeleza kilimo aliongeza" alisema
Mchinjita aliendelea na ziara yake katika Mkoa wa Morogoro ikiwa ni awamu ya pili ya ziara za chama hicho kuyafikia majimbo yote 214 ya bara ili kuandaa viongozi wao kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, vijiji na vitongoji unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED