Mbunge ataka mikopo itolewe bila usumbufu ‎

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:58 PM Feb 21 2026
‎Mbunge wa Viti Maalumu, Jasmin N'gumbi
Picha: Mpigapicha Wetu
‎Mbunge wa Viti Maalumu, Jasmin N'gumbi

‎Mbunge wa Viti Maalumu, Jasmin N'gumbi, mwakilishi wa vijana kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Iringa, amemuomba Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Fidelica Myovela, kuhakikisha mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu inatolewa kwa vikundi bila usumbufu wowote. ‎

 ‎Mbunge huyo alitoa rai hiyo wakati akichangia hoja katika Baraza la Madiwani kuhusu mapendekezo ya rasimu ya mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027. Alieleza kuwa kumekuwapo malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa vikundi vinavyoomba mikopo hiyo lakini kucheleweshewa au kunyimwa bila sababu za msingi.
 ‎
 ‎Amesisitiza kuwa mikopo hiyo ni haki ya makundi maalumu kwa mujibu wa sheria na miongozo ya serikali, hivyo halmashauri inapaswa kuweka utaratibu wazi, wa haki na unaoepusha urasimu usio wa lazima ili kuwawezesha wananchi kiuchumi.
 ‎
 ‎Awali akiwasilisha rasimu ya bajeti, Afisa Mipango na Uratibu wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Peter Ngusa, alisema halmashauri inakadiria kukusanya na kutumia jumla ya Shilingi 38,651,155,000 katika mwaka wa fedha 2026/2027.
 ‎
 ‎Alifafanua kuwa kati ya fedha hizo, Shilingi 8,844,800,000 zinatarajiwa kukusanywa kutoka mapato ya ndani, Shilingi 942,454,000 ni ruzuku ya matumizi mengineyo, Shilingi 23,376,336,000 ni ruzuku ya mishahara, na Shilingi 5,487,565,000 ni ruzuku kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
 ‎
 ‎Kwa mujibu wa bajeti hiyo, Halmashauri imejiwekea vipaumbele kadhaa, ikiwemo ununuzi wa maeneo ya uwekezaji, kuendeleza shamba la parachichi la Makalala, kuimarisha ujenzi wa miradi kimkakati pamoja na kuboresha ustawi wa wananchi kwa kuimarisha misingi ya utawala bora.
 ‎
 ‎Mbunge N’gumbi alisisitiza kuwa utekelezaji wa bajeti hiyo unapaswa kwenda sambamba na kuhakikisha makundi maalumu yanapata mikopo yao kwa wakati, ili kuchochea ajira na kukuza uchumi wa wananchi wa Mafinga.