Waziri wa Madini, Antony Mavunde, ameahidi kuwatoa wajasiriamali katika mikopo ya kaushadamu kwa kuwawezesha kupata mikopo yenye riba nafuu, lengo likiwa ni kuwainua kiuchumi kupitia biashara na shughuli za uzalishaji.
Ametoa ahadi hiyo leo Februari 18 katika hafla ya kukabidhi hundi ya Sh. bilioni mbili zilizotolewa kupitia Programu ya Imbeju, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Mtumba.
Amesema anatambua changamoto kubwa zinazowakabili wajasiriamali wengi, wakiwemo wale waliopokonywa mali kutokana na mikopo ya kaushadamu, hali inayowarudisha nyuma kimaendeleo.
“Najua kuna watu wanakaa chini, kuna wengine hawataki hata kuangalia taarifa za habari kwa sababu vitu vyao vimechukuliwa na watu wanaotoa mikopo ya kaushadamu. Nataka kuiondoa hali hiyo ili wajasiriamali mpige hatua,” amesema Mavunde.
Mavunde ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Mtumba, amesema moja ya ahadi zake kwa wakazi wa jimbo hilo ni kuhakikisha wanapata mikopo wezeshi yenye riba nafuu, ili waweze kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali za uzalishaji wanazozifanya.
“Naamini mikopo hii itawatoa kwenye mikopo ya kaushadamu. Naomba mliokidhi vigezo na wale mnaoelekea kupata mikopo hiyo tumieni vizuri na kuirejesha kwa wakati ili iendelee kutolewa kwa wengine,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Mwambapa, amesema taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha inawafikia wajasiriamali wengi nchini kwa lengo la kuwawezesha mitaji na mikopo kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.
Amesema Jimbo la Mtumba ni moja ya majimbo ya mfano, ambapo wajasiriamali zaidi ya 3,000 kupitia vikundi vyao watanufaika na mikopo ya Sh. bilioni mbili.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED