Makandarasi wametakiwa kuwa na uwazi wa thamani za ujenzi wa miradi katika mikataba yao

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:43 PM Oct 02 2024
Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi CRB ikiongozwa na Mwenyekiti Eng.Joseph Nyamhanga (wa nne kutoka kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Makandarasi CPP na SAMOTA wanaotekeleza Ujenzi wa Kituo cha Tano cha Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Masharika
Picha:Mpigapicha Wetu
Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi CRB ikiongozwa na Mwenyekiti Eng.Joseph Nyamhanga (wa nne kutoka kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Makandarasi CPP na SAMOTA wanaotekeleza Ujenzi wa Kituo cha Tano cha Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Masharika

Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi CRB, Mhandisi Joseph Nyamhanga ametoa wito kwa Makandarasi wote kuwa na uwazi wa thamani ya miradi ya ujenzi wanayotekeleza kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zote zinazoongoza shughuli za ujenzi hapa nchini.

Ametoa wito huo wakati wa ziara ya Bodi ya Wakurugenzi  na Menejimenti CRB ya kutembelea Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Africa Mashariki (EACOP) kutoka Kabaale – Hoima nchini Uganda kwenda kwenye peninsula ya Chongoleani mkoani Tanga nchini Tanzania, eneo la Igunga mkoani Tabora. 

“Wajibu wa CRB nikuhakikisha kuwa Makandarasi wote nchini wanaotelekeza miradi ya ujenzi kuwa na uwazi wa thamani ya miradi ya ujenzi pamoja na kuweka majina yao kwenye mabango ili pale CRB wanapopita kukagua waweze   kutambua ni Mkandarasi gani yupo kwenye mradi huo", alisema Mhandisi Nyamhanga.

Lengo la ziara hiyo  ni kujua maendeleo ya mradi na kujionea hatua mbalimbali za utendaji kazi, kuhakikisha kwamba kazi zote zinatekelezwa na Makandarasi waliosajiliwa na Bodi. 

Aidha Mradi huo unatekelezwa chini ya usimamizi wa Mkandarasi China Petroleum Pipeline Engineering Co. Ltd (CPP) umetoa mikataba kwa Makandarasi wa ndani Salum Motor Transport Co. Limited (SAMOTA) ambaye ni Sub Contractor.

“Ni jambo jema kuona kwamba kuna ushiriki mzuri wa Mkandarasi wa ndani katika mradi huu mkubwa ambao utawajengea uwezo na kushiriki katika shughuli mbali mbali katika mradi huu mkubwa wa mafuta ghafi kutoka nchini Uganda kuja Tanzania”, alisema Mhandisi Nyamhanga.

Mradi huu una urefu wa jumla ya kilomita 1443 kati ya hizo kilomita 296 zipo nchini Uganda na kilomita 1147 zipo Tanzania. Bomba linapita katika mikoa nane ya Tanzania Bara ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga. Bomba vilevile linapita katika wilaya 24, kata 134 na vijiji zaidi ya 180.