Makandarasi wametakiwa kushiriki miradi mikubwa ili kujijengea uwezo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:07 PM Oct 04 2024
 Makandarasi wametakiwa kushiriki miradi mikubwa ili kujijengea uwezo
Picha:Mpigapicha Wetu
Makandarasi wametakiwa kushiriki miradi mikubwa ili kujijengea uwezo

Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi CRB, Mhandisi Joseph Nyamhanga ametoa wito kwa Makandarasi wa ndani kushiriki kikamilifu katika miradi mikubwa inayotekelezwa hapa nchini ili kujijengea uwezo.

Ametoa wito huo katika  ziara ya Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya CRB wakati akikagua mradi wa Daraja la Kigongo - Busisi, unaotekelezwa kwa ubia na  Makandarasi China Civil Engineering Construction Cooperation (CCECC)  na China Railway Corporation (CRCC) jijini Mwanza.

Aidha Mhandisi Nyamhanga, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza  mradi huu ambao unakaribia kukamilika.

Sambamba na hayo ameridhishwa na Makandarasi CCECC  kwa kuajiri Mkandarasi wa ndani, kwa kufanya hivyo itawasaidia Makandarasi wa ndani kujijengea uwezo na kupata ujuzi mbali mbali.

“Naomba nitoe wito kwa Makandarasi wa ndani walio kwenye mradi huu na Makandarasi wote wa ndani kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa  miradi mikubwa  hapa nchini ili kupata ujuzi na kujijengea uwezo wa  makampuni yao ili waweze kutekeleza miradi mikubwa wenyewe," alisema Mhandisi Nyamhanga. 

Aidha Mhandisi Mshauri wa mradi huo Abdulkarim Majuto alisema kwamba hadi sasa ujenzi wa daraja hilo umefikia asiliamia 92.15 ya utekelezaji ambapo matarajio ni hadi kufikia tarehe 30/12/2024 utakua umeshakamilika.

Katika hatua nyingine Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya CRB ilifanya ziara katika Uwanja wa Ndege Mwanza na kukagua Mradi wa ujenzi wa jengo jipya la abiria , jengo la biashara, maegesho ya ndege, uzio wa usalama, kituo cha kupozea umeme, mifumo ya tehama na ya kuongozea ndege unaotekelezwa na Kampuni va Taifa Mining and Civil Limited.

Mhandisi Nyamhanga, amemtaka Mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi na kuiomba Mamlaka ya viwanja vya ndege Tanzania TAA kufanya malipo kwa wakati ili aweze kukamilisha ujenzi huo kwa mujibu wa mkataba.

Aidha Mhandisi msimamizi wa mradi Elikana Stanley kutoka TAA alisema gharama za mradi ni Bilioni 29.3 za mradi wote na  hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 60. 

Naye Mkandarasi anayetekeleza mradi huu wa uwanja wa ndege amehahidi kukamilisha ujenzi kwa wakati kwa mujibu wa mkataba wa kazi.

Pia Bodi hiyo, imefanya ziara katika Mradi wa ujenzi wa  majengo  ya Chuo cha Teknolojia ya Dar es salaam (DIT) tawi la Mwanza unaotekelezwa na Mkandarasi  Comfix and Engineering Limited.

Aidha Mwenyekiti wa Bodi Mhandisi Nyamhanga ameonesha kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo kutokana  na Mkandarasi kuwa nje ya muda wa mkataba wake.

"Maendeleo ya mradi huu uko nyuma na Mkandarasi tayari amekwisha pewa nyongeza ya mda mara tano na bado kazi haijakamilika, hivyo nitoe wito kwa Mkandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji ili ujenzi ukamilike ndani ya mda ulivopangwa" alisema Mhandisi Nyamhanga.

Pamoja na hayo amewataka Makandarasi wote nchini kukamilisha miradi waliyopewa kwa wakati uliyopangwa na kwa ubora unaotakiwa kwa kuzingatia gharama halisi kwa mujibu wa mikataba yao. 

Aidha kwa wale Makandarasi ambao hawatatekeleza kazi kulingana na mikataba walioingia, Bodi ya Usajili wa Makandarasi haitosita kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.