MAKANDARASI mkoani Shinyanga wameagizwa kutumia lugha ya Kiswahili kwenye mabango ya miradi ya ujenzi wanayotekeleza kwa manufaa ya wananchi.
Agizo hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki iliyopita wilayani hapa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha wakati akikagua ujenzi wa mradi wa barabara yenye urefu wa kilomita 12 ya uboreshaji wa miundombinu ya miji nchini (TACTIC).
Macha alifafanua kuwa ametoa agizo hilo kutokana na makandarasi kutumia Kingereza kwenye mabango yakionyesha ujenzi wa mradi unaendelea, isipokuwa neno moja tu UKIMWI linaandikwa Kiswahili.
Alisema mabango yanapoandikwa lugha ya kigeni, kunakuwapo sintofahamu ndani ya jamii kutokana na wengi wao kujiuliza anayejenga katika maeneo hayo.
Macha alisisitiza kuwa endapo mabango yataandikwa kwa Kiswahili itamrahisishia kila mwananchi kutambua kampuni, jina la mkandarasi, aina ya mradi kuanza kwake, kukamilika, gharama na mfadhili.
"Ninachokisema nimemaanisha, kuanzia miradi inayokuja nataka vibao viandikwe lugha ya Kiswahili ili wananchi waelewe na kuwaondolea maswali mengi dhidi ya miradi inayotekelezwa,” alisema na kuongeza kuwa:
“Tukumbuke siyo watu wote wanafahamu Kingereza, mambo haya yanaleta manung'uniko mengi juu ya miradi maana watu hawaelewi kinachoendelea."
Baadhi ya wakazi wa Majengo wilayani hapa, Magdalena Mussa na Ngassa Maige, kwa nyakati tofauti waliwataka makandarasi kuacha tabia ya kuwapa kazi wazawa wa maeneo hayo na kuwachukua watu kutoka maeneo mengine.
"Kuna kazi tunazoweza kufanya wananchi wa maeneo ulipo mradi, mfano kuwapikia chakula mafundi, kusogeza vifaa vya ujenzi mawe, mchanga na maji, lakini wanapatiwa watu kutoka maeneo mengine, sisi hatunufaiki na fedha za serikali zitokanazo na miradi kupitia ajira,” alisema Magdalena.
Maige, aliiomba serikali kuingilia kati suala la ajira na vibarua kwa wazawa katika miradi inayotekelezwa na serikali ili wananchi wa maeneo husika wanufaike na kuondokana na hali ngumu ya maisha.
“Sio kweli eti katika maeneo husika hawapo mafundi au vibarua wanaoweza kufanya kazi husika mpaka waletwe wa maeneo mengine, huu ni unyonyaji," alilalamika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED