Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeanza rasmi kuwaondoa wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika maeneo yasiyo rasmi, hatua inayolenga kurejesha utaratibu wa matumizi ya barabara na njia za waenda kwa miguu.
Uamuzi huo unatekeleza maagizo ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, aliyoyatoa wakati wa hafla ya ufunguzi wa Soko Kuu la Kariakoo. Katika hafla hiyo, mgeni rasmi alikuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Chalamila alisisitiza kuwa kurejesha barabara katika matumizi yake ya awali si jambo la hiari bali ni wajibu wa kisheria na kiutawala.
“Inawezekana lisiwe jambo zuri na yanaweza kuwa maelekezo machungu kwa wafanyabiashara, lakini huwezi kujenga nyumba yenye thamani ukaziba barabara. Naamini diplomasia itaendelea kutumika pasipo kutumia nguvu kwamba barabara zitabaki wazi,” amesema RC.
Kwa mujibu wa Chalamila, kuanza kwa huduma katika Soko Kuu la Kariakoo kutaambatana na kufunguliwa kwa barabara zote zinazoingia na kutoka sokoni hapo, ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kupunguza msongamano uliokuwa ukisababishwa na biashara kufanyika katikati ya njia.
Hatua hizo zilianza kuonekana wazi Februari 17, 2026, ambapo katika maeneo mbalimbali ya Kariakoo kulibandikwa matangazo rasmi yaliyosainiwa na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya. Katika matangazo hayo, wafanyabiashara waliokuwa wakipanga na kuuza bidhaa katikati ya barabara za mitaa na katika njia za waenda kwa miguu bila kupangiwa rasmi walitakiwa kuondoa bidhaa zao mara moja.
Operesheni hiyo inalenga kuhakikisha miundombinu ya jiji inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, hususan barabara na njia za watembea kwa miguu, huku wafanyabiashara wakihamasishwa kutumia maeneo rasmi yaliyotengwa kwa ajili ya biashara ndani ya soko.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED