Kibaha yapitisha Bajeti Mwaka 2026/27

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 04:57 PM Feb 18 2026
Akizungumza wakati wa kupitisha bajeti hiyo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dk. Mawazo Nicas.
Picha:Julieth Mkireri
Akizungumza wakati wa kupitisha bajeti hiyo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dk. Mawazo Nicas.

Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani wamepitisha bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 yenye jumla ya Sh.bilioni 68.7, katika Baraza Maalum la Madiwani lililofanyika Februari 18,2026.

Akizungumza wakati wa kupitisha bajeti hiyo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dk. Mawazo Nicas, amesema bajeti hiyo ni chachu ya maendeleo kwa wananchi na imezingatia mahitaji halisi ya halmashauri.

“Bajeti hii imepitia kamati zote, imejadiliwa na kuboreshwa. Ni wajibu wetu kuipitisha ili ikalete maendeleo kwa wananchi wetu,” amesema Dk. Nicas.

Diwani wa Kata ya Kibaha, Omary Bula, amesema bajeti hiyo imeandaliwa kwa ushirikishwaji wa madiwani wote na kuwataka wajumbe kuipitisha kwa maslahi ya wananchi.

Awali, Naibu Meya wa Manispaa ya Kibaha, Aziza Mruma, amewasilisha rasimu ya bajeti akieleza kuwa kiasi cha Sh.bilioni 68.7 kinawakilisha ongezeko la asilimia sita ukilinganisha na bajeti ya mwaka 2025/2026.

Mruma amefafanua kuwa mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh.bilioni 17.8, miradi ya maendeleo Sh.bilioni 8.7, huku asilimia 60 ya mapato ya ndani ikielekezwa kwenye miradi ya maendeleo na asilimia 40 kwenye matumizi ya kawaida. Aidha, Sh.bilioni 1.4 zimetengwa kwa ajili ya mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Katika mwaka huu wa fedha, Manispaa inatarajia kujenga kituo kimoja cha afya na zahanati mbili, pamoja na kutekeleza miradi ya kimkakati yenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.3. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa maegesho ya malori yenye thamani ya Shilingi Milioni 242.3, kituo cha kibiashara Mbonde, na kiwanda cha kusindika nyama chenye thamani ya Shilingi Milioni 524.7.

Baada ya majadiliano ya kina, madiwani kwa kauli moja waliipitisha bajeti hiyo, wakiahidi kusimamia utekelezaji wake kuhakikisha inaleta tija na maendeleo kwa wananchi wa Manispaa ya Kibaha.