Fedha zatengwa kujenga madaraja yaliyoharibiwa na El-Nino, kimbunga

By Gwamaka Alipipi , Nipashe
Published at 10:45 AM Sep 17 2024
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (wa pili kushoto), akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Pwani, Mhandisi Baraka Mwambage (wa pili kulia), alipokagua ujenzi wa barabara ya Nyamwage – Utete (Km 33.7)
Picha: Ida Mushi
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (wa pili kushoto), akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Pwani, Mhandisi Baraka Mwambage (wa pili kulia), alipokagua ujenzi wa barabara ya Nyamwage – Utete (Km 33.7)

SERIKALI imesema inatarajia kujenga daraja la mita 100 eneo la Mto Mbwemkuru mpakani mwa wilaya za Ruangwa na Kilwa pamoja na Daraja la Nakiu (mita 70) mkoani Lindi katika mwaka huu wa fedha.

Lengo la ujenzi huo ni kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa mkoa huo. 

Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, alieleza hayo juzi wakati akikagua miundombinu ya barabara na madaraja mkoani humo. 

Akiwa eneo hilo, Kasekenya alisema daraja la zamani ambalo limeharibiwa na mvua ya El- Nino na kimbunga Hidaya iliyonyesha mwanzoni mwa mwaka huu, litakarabatiwa na kutumika kwa muda wakati ujenzi wa daraja jipya ukiendelea. 

Kasekenya alisema: "Tutajenga daraja lenye urefu wa mita 100 hapa kutokana na ukubwa wa mto huu, tupo katika hatua za ununuzi za kumpata mkandarasi wa kujenga daraja hili, hivyo wananchi wa Lindi msiwe na wasiwasi kwani fedha zilishapatikana za kurudisha miundombinu hii." 

Aliongeza kuwa ujenzi wa daraja hilo unakwenda sambamba na ujenzi wa barabara ya Mtwara - Dar es Salaam pamoja na madaraja mengine yaliyoharibiwa na mvua hiyo na kimbunga Hidaya na kusisitiza kuwa hatua za kutafuta makandarasi zinaendelea na ujenzi wake unatarajiwa kuanza hivi karibuni. 

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, alipongeza Wizara ya Ujenzi kwa juhudi walizofanya, ikiwamo kurejesha mawasiliano kwa madaraja na barabara zilizoathiriwa na mvua ya El- Nino na kimbunga Hidaya mkoani humo kwa muda mfupi. 

Zainab alisema: "Nimpongeze Rais Samia Suluhu Hassan kwa serikali yake kutenga fedha kwa ajili ya kurejesha miundombinu hii, Wizara ya Ujenzi imekuja kufanya tathmini kuona maeneo yaliyoathirika, ninaamini utekelezaji utaanza mapema." 

Mvua ya El-Nino iliyonyesha mwaka jana, ilisababisha athari kubwa ya miundombinu katika mikoa mbalimbali nchini hususani mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Pwani.