EWURA: Msihifadhi wala kuuza mafuta ya petroli kwenye madumu, chupa

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 02:44 PM Sep 16 2024
Mafuta ya petroli kwenye chupa.
Picha: Mtandao
Mafuta ya petroli kwenye chupa.

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza kuanza ukaguzi kwenye vituo vya mafuta, ili kubaini vinavyokiuka sheria kwa kuuza petroli kwenye vifaa visivyoruhusiwa ikiwamo madumu na chupa za plastiki.

Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dk. James Andilile, ametoa kauli hiyo leo kwa umma kutokana na hivi karibuni kukithiri kwa matukio ya milipuko ya moto inayotokana na kuhifadhi ama kuuza mafuta ya petroli kwa kutumia madumu na chupa za plastiki, kinyume na tahadhari ya usalama wa afya, mali na mazingira.

Amesema kwa mujibu wa kanuni namba 27 ya kanuni zinazosimamia biashara ya vituo vya mafuta za mwaka 2022 kama ilivyochapishwa katika Gazeti la Serikali Namba 150, wamiliki wote wa vituo vya mafuta wanatakiwa kuchukua tahadhari kwa kuhakikisha kuwa usalama wa afya, mali na mazingira unazingatiwa ili kuepusha milipuko ya moto.

“Hivyo basi, mamlaka inawakumbusha wamiliki wote wa vituo vya mafuta kuzingitia matakwa ya Kanuni Namba 27 kwa kutoruhusu uuzwaji wa mafuta ya petroli kwenye vifaa visivyoruhusiwa kuchukulia/kuhifadhia mafuta kama vile madumu, chupa za aina zote na vifaa vingine visivyoruhusiwa kisheria,” amesema. 

Aidha, amesema EWURA inatoa tahadhari kwamba maofisa wake watafanya ukaguzi ili kubaini kama kanuni hiyo inazingatiwa ipasavyo na atakayebainika kukiuka atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria, ikiwamo kukifungia kituo husika.

Amesema: “Uuzaji mafuta kwenye vidumu na maeneo yasiyo rasmi unaweza kusababisha majanga ambayo yanagharimu maisha ya watu wengi hivyo nitoe wito kwa Watanzania wenzangu kuacha tabia hii ni hatari sana kwetu na kwa wale wanaotuzunguka.”