Dk. Jafo awataka wawekezaji kuzingatia uzalishaji wa bidhaa bora

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 06:34 PM Dec 17 2024
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo.

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo, amewataka wawekezaji kuzingatia uzalishaji wa bidhaa bora na zenye viwango ili ziweze kushindana kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi.

Dk. Jafo ametoa wito huo alipokagua mabanda ya bidhaa za viwandani katika Maonyesho ya Nne ya Biashara na Uwekezaji yanayofanyika Mailmoja, Kibaha.

Akizindua maonyesho hayo, Waziri Jafo amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wawekezaji kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili kuzalisha bidhaa bora.

Alipotembelea banda la Kampuni ya Kinglion, Waziri amepongeza kwa bidhaa zao bora huku akisisitiza umuhimu wa kuzalisha bidhaa zinazokidhi viwango vya kimataifa kwa ushindani wa soko.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge ameishukuru Kampuni ya Kinglion kwa kudhamini maonyesho hayo na kuahidi kushughulikia changamoto ya barabara katika eneo lao la uwekezaji ili kuhakikisha inapitika muda wote.

Meneja wa Kampuni ya Kinglion, Arnold Lyimo, ameishukuru Serikali kwa kuweka mazingira ya maonyesho ambayo huwapa fursa ya kuonyesha bidhaa zao.

Lyimo amebainisha kuwa kiwanda kipya cha kuzalisha malighafi za kutengeneza mabati kinachojengwa katika eneo la Viwanda Zegereni kinatarajiwa kuanza uzalishaji mwishoni mwa mwaka huu.

Amesema kiwanda hicho kikianza kazi kitazalisha tani 35,000 za malighafi kwa mwaka, huku kitarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja 1,500 na ajira za muda zaidi ya 5,000.

2