Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, amewataka watumishi wa Kituo cha Huduma Jumuishi (One Stop Center) wilayani Kishapu kuhakikisha wanatunza siri za wahanga wa ukatili wanapotoa taarifa ili kuepusha udhalilishaji.
Macha alitoa wito huo wakati wa uzinduzi wa kituo hicho, kilichojengwa kwa ufadhili wa UNFPA kupitia mradi wa "Chaguo Langu Haki Yangu", chini ya ufadhili wa Finland. Alisisitiza kuwa usiri utasaidia kuimarisha imani ya wahanga na kupunguza vitendo vya ukatili katika jamii.
Aliwataka wananchi kutumia kituo hicho kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia ili wahanga wapate huduma stahiki. Pia alikemea vitendo vya akina mama kuweka watoto mbele ya tenki la mafuta kwenye bodaboda, akisema hali hiyo inahatarisha afya zao.
Aidha, Macha aliwasihi wazazi kuhakikisha watoto waliofikia umri wa kuanza shule Januari 2025 wanapelekwa shule, huku akionya wazazi wanaowaficha watoto wenye ulemavu, akisema hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Dk. Godfrey Kisusi, alisema ujenzi wa kituo hicho ulianza Agosti 2023 na kukamilika Machi 2024 kwa gharama ya jumla ya shilingi milioni 178.2. Alibainisha kuwa tangu Machi hadi Desemba 2024, matukio 192 ya ukatili yamerekodiwa, yakiwemo ukatili wa kimwili, ngono, kisaikolojia na utelekezaji wa watoto.
Hata hivyo, Kisusi alieleza changamoto ya ukosefu wa nyumba salama kwa wahanga, hasa watoto waliopata mimba za utotoni, akisema hali hiyo inaharibu ushahidi kwani baadhi yao hurubuniwa wanaporudi nyumbani.
Mwakilishi Mkaazi wa UNFPA Tanzania, Mark Bryan Schreiner, na Mkuu wa Ushirikiano wa Ubalozi wa Finland, Juhana Lehtinen, walisisitiza kuwa kituo hicho kitatoa msaada mkubwa kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia, hususan wanawake, watoto, na watu wenye ulemavu, huku wakiahidi kuendelea kushirikiana na serikali kupambana na ukatili na kuimarisha usawa wa kijinsia.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED