Biteko aonya watu kusaka uongozi kwa fedha

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 06:55 AM Sep 15 2024

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.
Picha: Mtandao
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, ameonya watu wanaotumia fedha kusaka uongozi wakati wa uchaguzi.

Amesema katika kuelekea kipindi cha uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba, mwaka huu, na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani, mtu kuwa na fedha isiwe sehemu ya  sifa ya kupata uongozi. 

Alisema hayo jana wakati akifunga maonesho ya saba ya kitaifa ya Mifuko ya Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yaliyokuwa yakifanyika mkoani Singida kuanzia Septemba 8 hadi 14, mwaka huuu. 

Biteko ambaye alimwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema akitokea mtu ambaye hana fedha na hali yake ni ngumu kimaisha lakini ana mawazo mazuri ya kuwaongoza wananchi kwenye mitaa,kitongozi au kijiji wananchi wamchague. 

"Sifa ya kuchagua kwa sababu ya mtu mwenye fedha naomba isiwe sehemu ya kwenye uchaguzi huu,tuchaguane kwa sifa,tusichaguane sababu ya ukabila huyu ni Mnyaturu mwenzangu au Mnyiramba mwenzangu,tuchaguane kwa sababu ya uwezo," alisema. 

Alisema wananchi wasifanye kosa kuchagua viongozi ambao hawana uchungu na maendeleo yao na taifa kwa ujumla. 

Dk. Biteko alisema uchaguzi wa serikali za mitaa si uchaguzi mdogo ni mkubwa kwa maendeleo ya nchi hivyo wachaguliwe viongozi wanaojua shida za watu. 

"Wewe uliyesoma au wewe mwenye takriba ya juu sasa usione uchaguzi huu haukuhusu ni uchaguzi muhimu wa kutafuta viongozi wanaojua shida za watu kuanzia Januari hadi Desemba, kuanzia Jumatatu hadi Jumapili na kuanzia saa moja asubuhi hadi saa moja jioni," alisema. 

Aliongeza kuwa ili serikali iwawezeshe wananchi kiuchumi lazima kuwe na viongozi ambao wana uchungu na maendeleo ya watu ambao wakiamka wanawaza tu maendeleo.

 "Wako madiwani wanahitaji viongozi wa serikali za mitaa wazuri ambao watabeba shida za wananchi zinazowakabili. Mkichagua  viongozi kwa kuangalia kwamba tunaabudu pamoja au ana uwezo wa kifesha, mtakuwa hamwatendei haki watoto wa watoto wenu ambao watakuwa wanaamini sifa bza kifedha,ukabila na udini zimewapa nafasi ya kuwa viongozi," alisema.

 Biteko alisema mwaka huu Mifuko ua Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi imepiga hatua kubwa kiuchumi kwa kuwafikia watanzania wengi zaidi na kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu.

 Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, alisema zaidi ya Sh. bilioni 2.5 ziko benki na zitatumika kutoa mikopo kwa wanawake, vijana na makundi maalum kwenye halmashauri za wilaya za mkoa wa singida. 

 Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi, Being' Issa, alisema maonesho hayo mwakani yatafanyika mkoani Mwanza.