Benki ya Mkombozi yakuza mikopo kutoka bil 28.8/- hadi bil 134.3/-

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 08:02 PM Jun 17 2024
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Chande (wa pili kutoka kulia) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Respige Kimati (katikati), pamoja na wageni wengine katika hafla hiyo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Chande (wa pili kutoka kulia) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Respige Kimati (katikati), pamoja na wageni wengine katika hafla hiyo.

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya Biashara Mkombozi, Gasper Njuu, amesema kwa kipindi cha miaka 15 tangu kuanzishwa kwa benki hiyo, malengo ya benki, ikiwamo utoaji kwa Mtanzania, yamefanikiwa.

Imekuza kiwango cha utoaji mikopo kutoka Sh. bilioni 28.8 Desemba mwaka 2013 hadi kufikia Sh. bilioni 134.3 mwaka jana, ikiwa ni ongezeko la asilimia 36 kwa mwaka.

Amesema benki hiyo imeweza kutoa huduma za kibenki hasa mikopo midogo, kwa watu binafsi wakiwamo vijana na wanawake, kwa kuwapatia mikopo ya kati pamoja na mikubwa kwa makampuni, taasisi za huduma na wafanyabiashara.

Gasper aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, wakati benki hiyo ikitangazwa rasmi kupandishwa daraja na kuorodheshwa kwenye benki ya biashara katika soko la hisa.

“Safari yetu katika Soko la Hisa la Dar es Salaam  Daraja la Soko la Ujasiriamali, imekuwa yenye mafanikio makubwa. Tumeshuhudia ukuaji mkubwa wa faida, ongezeko la amana za wateja, ongezeko la mikopo iliyotolewa kwa Watanzania.

“Hii ni benki ya watu wote bila kujali itikadi zao za siasa, rangi, kabila au dini, tangu kuanzishwa kwa benki miaka 15iliyopita, kulikofuatiwa na kuorodheshwa kwa Benki katika Soko la Hisa la Dar es Salaam miaka 10 iliyopita,” alisema Gasper.

Alisema benki hiyo imetoa ajira kwa Watanzania, mikopo iliyochochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi, imeshiriki moja kwa moja na mara kwa mara katika shughuli za kijamii na serikali imefaidika na kodi mbalimbali zinazotokana na utendaji wa benki hii. 

“Mpaka kufikia Desemba 2023 benki hii ilikuwa na jumla ya wafanyakazi 185 kwa uwiano wa kijinsia wa wanawake 82 na wanaume 103. Tunapoingia katika hatua hii mpya ya kuwa sehemu ya Soko Kuu la Uwekezaji (MIMS) katika Soko la Hisa la Dar es Salaam, tunayo imani kubwa kwamba mafanikio zaidi yanakuja mbele yetu.”

Aliongeza kwamba wadau mbalimbali wawaunge mkono, ikiwamo watunga sera katika safari ya maendeleo, ili kuhakikisha malengo ya muda mrefu yanatimia pamoja na kuboresha huduma kwa wateja. 

Awali, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Chande aliipongeza hiyo kwa kupanda hatua moja kwenda nyingine ndani ya muda mfupi, huku amewasihi watendaji kutoridhika na hatua waliyofikia.

“Hongereni sana Mkombozi Bank kwa hatua hii mliyofikia, kwa sababu mmepanda hadhi kutoka hatua moja kwenda nyingine ndani ya muda mfupi sana. Lakini niwaombe, msiridhike na hatua hiyo mliyoifikia.

“Endeleeni kuhamasisha ili benki hii ya Mkombozi iendelee kukua. Kwa hiyo naomba kutangaza rasmi kwamba Mkombozi Benki mepandishwa rasmi kutoka Soko la Ujasiriamali (EGM) na kuingizwa Katika Soko Kuu la Uwekezaji (MIMs),” alisema Naibu Waziri.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Mkombozi, Respige Kimati, alisema kuwa benki hiyo, imekuwa mstari wa mbele kuungana na serikali katika kuwashika mkono watu waliopatwa na majanga mbalimbali ndani ya jamii.

Kimati alisema wateja, wanahisa, mamlaka mbalimbali za usimamizi wa sekta ya fedha nchini na watunga sera, waendelee kuwaunga mkono katika safari, kuhakikisha wanatimiza malengo ya muda mrefu na kuboresha huduma.