RC aagiza msako watuhumiwa ulawiti, ubakaji watoto

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:59 PM Jun 26 2024
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Buriani.
Picha: Maktaba
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Buriani.

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Buriani, ameagiza kufanyika msako maalum usiku na mchana wa kuwatafuta watuhumiwa wa ubakaji na ulawiti, waliowafanyia watoto wanane kwa kuwarubuni wakiwa kwenye kibanda cha kukaangia mihogo.

Watoto hao wanadaiwa kubakwa na kulawitiwa, wakiwa jirani na shule yao iliyoko Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga.

Ametoa agizo hilo juzi, alipokwenda kuzungumza na madiwani wa Wilaya ya Muheza, waliokuwa wakiendelea na kikao maalumu cha baraza la madiwani, lililoketi kupokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Pamoja na mambo mengine, amelaani kitendo hicho na kuagiza kufanyika kwa kura za siri, ili kubaini watu wote wanaounga mkono vitendo hivyo.

Pia, amelitaka Jeshi la Polisi mkoani hapa kutolala na wajitume kuwasaka watuhumiwa hao hadi wapatikane katika kipindi cha muda mfupi kuanzia sasa.

Vilevile, amesema kitendo cha aina hiyo pia kimeripotiwa katika Wilaya ya Mkinga, huku akiitaka jamii kufunga kibwebwe kupambana na vitendo hivyo, kwa kuwa kama vikiachwa vinaweza kuathiri kizazi cha sasa na baadaye.

Balozi Dk. Burian, amesema kuwa iwapo uchunguzi utafanyika na akapatikana mtu yeyote, awe mwalimu au kiongozi wa dini yeyote, hawatamwacha kwani vitendo hivyo vimekuwa vikidhoofisha nguvu kazi ya taifa.

Amesema: “Watu wazima wameanzisha kigenge cha makusudi cha danganya toto, kumbe wana shughuli zao nyingine watoto wakienda wanadanganywa na mihogo ya kukaanga, wanawadhulumu watoto wadogo wa kike wa miaka 8, 9 mpaka 10. Huyo wa mwisho alienda akapatwa na changamoto ya kutokwa na damu nyingi kwa kuwa alikuwa ni mdogo ndiyo watu wakajua”.