Msonde ataka kasi ujenzi jengo la wizara

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 07:31 AM Sep 28 2024
Msonde ataka kasi ujenzi jengo la wizara
Picha:Mtandao
Msonde ataka kasi ujenzi jengo la wizara

NAIBU Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Dk. Charles Msonde amemwagiza mkandarasi anayejenga jengo la wizara hiyo kuhakikisha anapanga ratiba maalum ya utekelezaji mradi huo ili iendane na kasi ya muda wa nyongeza aliopewa.

Alitoa maagizo hayo juzi baada ya kukagua ujenzi huo unaotekelezwa katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, akiwa pamoja na Menejimenti ya Wizara hiyo.

Dk. Msonde alimtaka mkandarasi huyo kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana ili jengo hilo likamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

"Wekeni mpango mkakati maalum wa utekelezaji kazi zenu ili uendane na muda mliopangiwa, hakuna sababu ya kuchelewesha mradi huu, kwani kila kitu mnacho, kumbukeni hakutakuwa tena na muda wa nyongeza," aliagiza.

Dk Msonde pia alimtaka Mhandisi Mshauri  anayesimamia mradi huo, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuhakikisha anausimamia mara kwa mara ili kuangalia maendeleo yake na kubaini mapema changamoto zitakazojitokeza na kutafutiwa ufumbuzi wa haraka.

Alimsisitizia mkandarasi huyo kufanya kazi kwa uaminifu na weledi ili kuaminika na kupatiwa kazi nyingi zaidi ambazo zitatangaza taasisi hiyo.

Meneja Mradi kutoka vikosi vya ujenzi wanaotekeleza mradi huo, Stanslaus Mkude, alimhakikishia Naibu Katibu Mkuu, kufanya kazi kwa ubora na kuweka ratiba maalum itakayosaidia kumaliza mradi huo kwa wakati.

Alisema jengo hilo kwa sasa limefika asilimia 76 ya ujenzi wake na kinachofanyika ni kumalizia uwekaji wa vigae na kufunga vioo katika maeneo mbalimbali ya jengo hilo.