TPDC kuendelea kutafiti wa mafuta Bonde la Eyasi Wembere

By Zanura Mollel , Nipashe
Published at 04:40 PM Sep 26 2024
Meneja Mradi  wa Utafutaji Mafuta na Gesi ya asili Bonde la Eyasi Wembere
Picha: Mpigapicha Wetu
Meneja Mradi wa Utafutaji Mafuta na Gesi ya asili Bonde la Eyasi Wembere

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania(TPDC) linaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ya serikali ikiwemo mradi wa utafiti wa mafuta katika Bonde la Eyasi Wembere.

Meneja Mradi  wa Utafutaji Mafuta na Gesi ya asili Bonde la Eyasi Wembere wilayani Meatu Mkoa wa Simiyu, Sindi Maduhu amesema kiasi cha shilingi bilioni 43 kimetengwa kwa ajili ya kutekeleza mradi huo katika mikoa mitatu, wilaya tano na vijiji 17 vilivyopo katika Bonde la Ufa.

"Lengo la kuitafuta rasilimali ya mafuta ni kuimarisha uchumi wa Taifa,Mikoa hiyo ni  Simiyu wilaya ya meatu, Arusha wilaya za Ngorongoro na Karatu pamoja na Singida wilaya za Iramba na Mkalama" anasema Maduhu

Hapo Jana akizingumza na wanahabari  amesema mradi wa uchukuaji wa taarifa za nyongeza za mitetemo ya mfumo wa 2D itachukua zaidi ya miaka miwili kwa kumtumia mkandarasi  kampuni  ya African Geophysical  Services(AGS) mwenye mitambo maalum ya mitetemo.

Aidha Maduhu amesema mradi huo umekua sehemu ya kuchochea maendeleo kwa mtu mmoja mmoja kwa kuwa asilimia zaidi ya 70 ya wafanyakazi wake ni wazawa huku asilimia chini ya 30 ikiwa ni raia kutoka Nje ya nchi.

Ramani ya Mradi.
Hata hivyo ametoa wito kwa wakazi wa eneo hilo hususani katika kata Bukundi, Mwanjolo, Kidaru, Mpambala, Mwangeza, Mwamalole na Baray kutohujumu mradi huo kwa kuiba au kung'oa vinasa sauti vinavyowekwa kwa lengo la kukusanya taarifa za mitetemo na kuwahasa kuwa mabalozi wazuri katika utekelezaji wa mradi huo .

Naye Kaimu Meneja wa Kampuni ya AGS inayofanya kandarasi katika mradi huo Brian Kamoga  amebainisha kuwa mradi huo umejikita katika matumizi ya Teknolojia ya kisasa ikiwa ni sehemu ya takwa la serikali katika kukimbiza Kasi ya Maendeleo.