Samia ataka wanaoharibu amani wapuuzwe

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 10:42 AM Sep 26 2024
Rais Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan amewasihi Watanzania kuwapuuzia wanaowashawishi kuharibu amani ya nchi kwa sababu zozote kwa kuwa kufanya hivyo kunarudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Mbinga akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake mkoani Ruvuma na kuzindua jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.

Pia alitembelea kituo cha ununuzi mahindi na soko la Jimbo la Mbinga Mjini, aliweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Bandari ya Mbambabay na kufungua barabara ya Mbinga-Mbambabay yenye kilometa 60 iliyojengwa kwa kiwango cha lami.

Aliwasisitiza wananchi wa Mbinga wawapuuze wanaokwenda kuwashawishi kuharibu amani ya nchi kwa kuwa watu hao hawana nia njema, bali wanalenga kuharibu taswira ya nchi.

Alisema pamoja na changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi, Tanzania ni sehemu salama ya kuishi akiita kuwa ni "pepo" kulinganisha na nchi nyingine.

"Ninataka kuwaambia kwamba wameishiwa, hawana pa kupenya, wameshaona mbele mambo magumu kwao, sasa la kufanya ni kuharibu amani na utulivu wa nchi yetu, ili wananchi waishi kwa shaka, mwone nchi yenu si njema, ndio lengo lao," alisema.

Rais alisema nchi inapokuwa na amani na utulivu, maendeleo hufanyika vizuri kwa sababu wananchi watakuwa na uhuru wa kufanya shughuli za maendeleo.

Akikagua jengo la Halmashauri ya Mbinga, Rais alisema kukamilika kwake kutarahisisha utoaji huduma kwa wananchi kwa kuwa maofisa kutoka idara mbalimbali watapatikana eneo moja.

Aliwaagiza viongozi wa wilaya kuwapa elimu wakulima juu ya madhara ya kuuza mazao yao kwa mawakala ikiwamo kulanguliwa, hivyo kukosa fedha za akiba na kujiinua kiuchumi.

Alisema mawakala hao wamekuwa wakinunua mahindi kwa wakulima kwa Sh. 300 kwa kilo kisha kwenda kuuza Sh. 700 bei ambayo mkulima anauza kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).

Rais pia alisema serikali inaendelea kutoa vibali vya kuongeza watumishi wa afya kadri bajeti inavyoruhusu ili kuziba pengo la uhitaji wa watumishi hao katika wilaya hiyo.

Pia alimwagiza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, kupeleka wataalamu wa vizimba vya samaki katika wilaya hiyo na kuwafundisha wafanyabiashara teknolojia hiyo, ili serikali inapofunga shughuli za uvuvi kwenye maziwa kwa muda wasiathirike kiuchumi.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aliwaahidi wakulima wa eneo hilo kuwa kuanzia mwakani, vituo vyote vya NFRA vitakuwa na mashine za kisasa za kusafisha mahindi, hivyo wakulima hawatosafisha kwa mikono kama wafanyavyo sasa.