Zanzibar kuimarisha ushirikiano na Kituo cha Utafiiti wa Mboga Mboga Arusha

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:19 PM Sep 26 2024
Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili Na Mifugo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Shamata Shaame Hamisi (kushoto) akiongozana na Mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mboga Mboga kanda ya Afrika Dk. Gabriel Rugalema (katikati)...
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili Na Mifugo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Shamata Shaame Hamisi (kushoto) akiongozana na Mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mboga Mboga kanda ya Afrika Dk. Gabriel Rugalema (katikati)...

Ikiwa ni sehemu ya kuimarisha na kuboresha sekta ya kilimo hususani sekta ndogo ya mboga mboga na matunda pamoja na kuongeza usalama wa chakula, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeelezea utayari wake wa kuongeza kasi ya ushirikiano na Kituo cha Utafiti wa Mboga Mboga kilichopo jijini Arusha (World Vegetable Center).

Hayo yalisemwa na Mheshimwa Shamata Shaame Hamisi,Waziri na Katibu Mkuu  wa Wizara ya Kilimo Umwagiliaji, Maliasili Na Mifugo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati alipotembelea ofisi za kituo kwa kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika zilizopo jijini Arusha.

Kituo hicho kimekuwa kikifanya kazi na Zanzibar kwenye sekta ya kilimo hususani kwenye mboga mboga na matunda katika maeneo mbali mbali ikiwemo utafiti, mafunzo pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa kilimo na wakulima.

Waziri Shaame alisema ziara yake hiyo inaonesha uhusiano imara unaoendelea kukua kati ya Kituo cha Utafiti wa Mboga na Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili Na Mifugo ya Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha kilimo endelevu, ushirikiano katika utafiti, na kuendeleza sekta ya mazao ya mboga, matunda, viungo na vikolezo nchini Tanzania.

Katika ziara hiyo, Mhe. Waziri na Katibu Mkuu walipata fursa ya kutembelea miundombinu ya kisasa ya utafiti ya Kituo cha Utafiti wa Mboga Mboga, ikiwa ni pamoja na benki ya vinasaba (genebank), maabara, mashamba ya majaribio yanayoonesha aina mbali mbali za mboga mboga, pamoja na kituo atamizi cha vijana cha ujasiriamali.

Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili Na Mifugo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Shamata Shaame Hamisi akiumwagilia mti alioupanda muda mfupi baada ya ziara yake ya kikazi katika Kituo cha Mboga Mboga na Matunda cha Arusha. Wanaosuhudia ni Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo Zanzibar Dk. Mohammed Dhamir wa kwanza kushoto akifuatiwa na Mkurugenzi wa Kituo cha Mboga Mboga kanda ya Afrika Dk. Gabriel Rugalema, Mkurugenzi Mkaazi wa Tanzania Colleta Ndunguru wa kituo, Katibu Mkuu Kilimo Zanzibar Ali Khamisi Juma na Idris Hassan Abdullah kutoka kilimo Pemba.
Akiongea kuhusu ziara hiyo Mkurugenzi mkaazi wa kituo hicho Colleta Ndunguru alisema mazungumzo katika ziara hiyo yalijikita maeneo kadhaa ya ushirikiano yanayolenga kuimarisha sekta ya kilimo Zanzibar, hususan kilimo cha mboga mboga, na kuboresha usalama wa chakula.

“Maeneo hayo ni pamoja na ukusanyaji na uhifadhi wa rasilimali za vinasaba vya mimea, kuimarisha mnyororo wa thamani na kukuza masoko, utoaji mafunzo na ushirikiano katika utafiti, na kupeana taarifa ya miradi. Aidha, ushirikiano huu unalenga kuunganisha wakulima na sekta ya utalii, hasa hoteli, ili kukuza uzalishaji wa kilimo ndani ya Zanzibar na kupanua fursa za masoko kwa wakulima wa ndani,” alisema
Mtaalamu wa uandaaji na uzalisha wa mbegu bora kutoka Kituo cha Kimataifa cha Mboga Mboga na Matunda cha Arusha Dk. Fekadu Dinsa akifanua jambo kwa Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili Na Mifugo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Shamata Shaame Hamisi (kati kati) wakati alipotembea kituo hicho. Kulia ni Mkurugenzi Mkaazi wa kituo kwa Tanzania Colleta Ndunguru.

Aliongeza kuwa kituo cha Utafiti wa Mboga Duniani kitajikita katika programu yake ya mafunzo kwa maana ya African Vegetable Training Course (AVTC) ili kuimarisha uwezo wa wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili Na Mifugo Zanzibar na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar (ZARI) kwa kuboresha ushirikiano wa uzoefu, maarifa na utafiti.

Kwa upande wake Waziri Shaame alikishukuru kituo kwa kufungua milango ya ushirikiano na Zanzibar na kusema kuwa ushirikiano huo siyo tu unasaidia kuboresha kilimo kisiwani humo bali pia usalama wa chakula kwa watu wa Zanzibar.

PICHA.