MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amesema amewasiliana na mwanasheria wake kufungua kesi dhidi ya kampuni ya mawasiliano ya simu ambayo inadaiwa kuvujisha mawasiliano yake ya simu, hata kufanikisha shambulio la kupigwa risasi miaka saba iliyopita.
Ni hatua anayokusudia kuchukua baada ya gazeti la The Guardian la Uingereza juzi kuripoti kesi inayoendelea mahakamani nchini humo iliyofunguliwa na aliyekuwa Ofisa Usalama wa kampuni hiyo ya mawasiliano dhidi ya kampuni mama kwa kumwachisha kazi kutokana na anachodai kufanya uchunguzi dhidi ya wafanyakazi waliovujisha taarifa hizo.
Lissu ambaye alishambuliwa kwa risasi (inadaiwa risasi 38 zilielekezwa kwake akiwa katika gari lake) Septemba 7, 2017, kwenye eneo la nyumba za viongozi wa serikali jijini Dodoma, alitangaza hatua hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam kuhusu kesi hiyo inayoendelea jijini London, Uingereza.
"Wamesema walikuwa wanatuma taarifa kwa njia ya WhatsApp, baadaye serikali ikawaambia wafute, itabidi wataalamu watuambie kama kuna uwezekano wa kurejesha taarifa zilizofutwa.
"Itabidi watuambie majina na itakayotuambia ni... (anataja jina la kampuni hiyo ya mawasiliano). Kampuni mama si wako Uingereza, tutaanza nao. Hatutakwenda kwenye mahakama za hapa. Tutakwenda Uingereza.
"Tukienda huko nimewaambia walianzishe, leo (jana) nimezungumza na Robert Amsterdam, nimemwambia una mamlaka kamili ya kulianzisha. Hatujazungumza madai ya fedha, ninafikiri yatakuwa mengi sana, hatujayajadili bado," alisema.
Lissu aliendelea: "Tunataka majina na vyeo, kama (anataja kampuni) walilipwa, tunataka watuambie. Tunataka tujue hawa wanaoitwa watu wasiojulikana kwa miaka saba ni kina nani?
"Tunataka hiyo taarifa tujue nani alifanya nini na lini? Kwa sasa tuna mahali pa kuanzia. Tumepata ushahidi ambao hatukuwa nao, kuna kazi kubwa ya kufanya sasa hadi kufungua kesi."
Lissu alisema tukio hilo katika tafsiri ya sheria, ni kitendo cha ugaidi kwa mujibu wa sheria za Tanzania; alipata ulemavu wa kudumu, hawezi kutembea sawasawa.
Alisema anatembea na risasi mgongoni na mwili umejaa vyuma kwenye goti mpaka kwenye nyonga, makovu ya risasi 16 zilizompata kati ya 38 na ya operesheni 25.
Lissu alisema watoto wake hawajarudi Tanzania miaka mitano na juzi walimpigia, wakimwambia wanapenda kurudi nyumbani, lakini walifikiria walivyomwona Nairobi, Kenya wanashindwa kurejea.
"Mke wangu ameshindwa kurudi nyumbani ameogopa. Mimi king’ang’anizi tu. Tunahitaji kuambiwa ukweli wote," alisema.
WALIOMPIGA RISASI
Lissu alidai vijana wawili waliompiga risasi wapo na wajulikana na kwamba muda ukifika atawataja, huku akitaja jina la kiongozi mmoja wa kisiasa kuwa ndiye aliongoza kikosi kumshambulia.
"Kwa sheria yetu, Katiba yetu, serikali haina rukhsa ya kupewa mawasiliano ya wateja, mtu ana haki ya faragha, polisi hawatakiwi kuchunguza mawasiliano ya raia.
"Kuanzia siku hiyo na miaka yote mpaka leo (jana), serikali siku zote imesema kwamba, hao walionishambulia katikati ya majengo ya serikali ni watu wasiojuliana.
"Serikali wakati ule kwa sababu sikuwapo nchini nikiwa nje kwa matibabu, walidai kwamba watalichunguza nitakaporudi Tanzania.
"Hawajachunguza mpaka sasa hivi, hata kuitwa polisi kuulizwa 'hebu tuambie umeona nini?' Niliona vijana wawili walionishambulia. Lakini kuitwa na polisi kusema niliona nini, hata hilo hawajawahi kufanya.
"Ninaamini hawajawahi kufungua hata jalada. Watu walionipeleka hospitalini, walikuwa ni pamoja na mtumishi wangu wa nyumbani, yuko Dodoma na mfanyakazi wa Bunge aliyekuwa akifanya kazi katika makazi ya (Naibu Spika wa Bunge wakati huo), Dk. Tulia Ackson, na wao hawajawahi kuhojiwa," alidai Lissu.
FEDHA MATIBABU
Lissu pia alisisitiza kauli yake ambayo huitoa kila mara akidai kwamba: "Sijawahi kulipwa hata senti moja ya matibabu. Sheria ya Uendeshaji Bunge ilitungwa mwaka 2008, inasema mbunge akiugua, serikali inawajibika kumpa matibabu ndani au nje ya nchi."
Mtaalamu huyo wa sheria pia alikumbushia stahiki zake za matibabu kwa kuwa alikutwa na tukio hilo akiwa mbunge, na kwamba amekuwa akiombwa nyaraka mara kwa mara na serikali lakini hawajatimiza.
RIPOTI YA THE GUARDIAN
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na gazeti The Guardian la Uingereza, aliyekuwa Ofisa Usalama wa kampuni hiyo ya mawasiliano ya simu, amefungua kesi nchini humo akidai kufukuzwa kazi bila haki baada ya kupinga hatua ya kutoa data za simu za mwanasiasa Tundu Lissu mwaka 2017 na kuvujishwa bila ridhaa yake.
Anadai kuwa akiwa mfanyakazi wa kampuni hiyo, alivutiwa na mazungumzo fulani yaliyofanyika kwenye mkutano wa mtandaoni na yeye akiwa mshiriki, na kwamba alishtuka kwamba kuna jambo linaendelea pasipo yeye kushirikishwa kama mkuu wa idara.
Anadai alianzisha uchunguzi binafsi na kubaini kulikuwa na mawasiliano yasiyo ya afya baina ya kampuni na idara fulani ya serikali, ambayo yalifanyika kupitia mtandao wa WhatsApp, kampuni hiyo ya simu ikivujisha taarifa binafsi za simu za Lissu.
"Uvujishaji ulianzia tarehe 22 Agosti 2017, lakini kuanzia Agosti 29, 2017 kukawa na uvujishaji mkubwa wa taarifa za Lissu mbashara (live tracking). Taarifa hizo zilihusu maeneo aliyopo Lissu, simu zinazoingia na kutoka zikisikilizwa na SMS (ujumbe) zake zikisomwa.
Anadai kuwa mawasiliano yale yalifutwa bila kuwapo nyaraka inayoelekeza vile na ndipo aliamua kuandika ripoti maalum juu ya alichobaini na kuwasilisha kwa wakuu wake akiwajulisha ana shaka kampuni yake ilishiriki kumuuza Lissu kwa watu waliokuwa na kiu na damu yake.
Badala ya suala hilo kufanyiwa kazi, Novemba mwaka huo alifutwa kazi kwa kigezo cha kupunguzwa kazini, lakini anaamini uchunguzi alioanzisha ulikuwa nyuma ya yote yaliyomtokea ndipo aliamua kwenda kudai haki mahakamani.
Nipashe ilimtafuta Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba, ambaye baada ya kuelezwa kuhusu suala hilo, alitaka atumiwe ujumbe wa maandishi. Alitumiwa, lakini hakujibu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED