Mwalimu mbaroni tuhuma za kumuua mwanafunzi

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 12:14 PM Sep 26 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda.
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda.

ADRIAN Tinchwa (36), Mwalimu wa Shule ya Msingi Igurwa na Mkazi wa Kanoni, wilayani Karagwe, mkoani Kagera anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma za kumshambulia na kumsababishia kifo Mwanafunzi Phares Buberwa, akimtuhumu kumwibia simu.

Mwanafunzi huyo aliyekuwa akisoma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Igurwa, anadaiwa kukutwa akitoka ndani kwa mwalimu huyo (mtuhumiwa) ambaye alikuta kufuli la nyumba limevunjwa.

Akitoa taarifa ya kukamatwa kwa mwalimu huyo juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda alisema mtumishi huyo wa umma anadaiwa kumshambulia mwanafunzi huyo kwa kumpiga ngumi kwenye paji la uso kisha kutumia nondo kumpiga nayo miguuni na mikononi akimtuhumu kumwibia simu yake.

Kamanda Chatanda alisema tukio hilo lilitokea Septemba 18, 2024, saa nane mchana katika Kijiji cha Kanoni, wilayani Karagwe.

"Awali tarehe hiyo hiyo majira ya saa tatu asubuhi, inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alifika nyumbani kwake na kukuta kufuli la mlango wa nyumba yake limevunjwa na alipotaka kuingia ndani alikutana na Phares Buberwa, mlangoni akijaribu kukimbia," alisema Chatanda.

Alisema kuwa baada ya hapo alimkamata na kuanza kumshambulia hadi kumsababishia majeraha makubwa mwilini mwake na baadaye kumpeleka hadi nyumbani kwa wazazi wake na kumkabidhi kisha wazazi wake walimpeleka katika Kituo cha Afya cha Rwambaizi kwa ajili ya kupata matibabu.

"Phares alifariki dunia kituoni huko wakati akipatiwa matibabu na chanzo cha tukio hili ni mtuhumiwa kujichukulia sheria mkononi na kutoa adhabu iliyopitiliza kwa marehemu huyo hadi kufikia hatua ya kukimbizwa kituo cha afya," alisema Kamanda Chatanda.

Alisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara tu baada ya taratibu zote kukamilika.

"Wito wangu kwa wananchi ni kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi badala yake wafuate taratibu zote za kisheria pindi wanapokamata wahalifu kwani hatutasita kuwachukulia hatua wote watakaoshindwa kufuata sheria kwani hakuna aliye juu ya sheria," alisema Kamanda Chatanda.