Rais Ruto aapa kutokomeza maandamano ya vurugu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:38 PM Jun 26 2024
RAIS wa Kenya, William Ruto.
Picha: Maktaba
RAIS wa Kenya, William Ruto.

RAIS wa Kenya, William Ruto amelihutubia taifa usiku wa kuamkia leo ambapo amesema kuwa maandamano ya kupinga ongezeko la kodi na ushuru yalivamiwa na makundi ya wahalifu hivyo ameapa kuwa matukio kama hayo hayatajirudia tena.

Ruto ameapa kwamba matukio ya uvamizi wa Bunge aliyoyaita ‘kitisho kwa usalama wa taifa’, kamwe hayatojirudia kwa gharama yoyote. Hayo yanajiri wakati jumuiya ya kimataifa ikielezea wasiwasi wake kutokana na hali ya vurugu inayoshuhudiwa nchini humo.

Kupitia televisheni, DW imeripoti kuwa, Rais William Ruto wa Kenya ameapa kuchukua msimamo mkali dhidi ya "vurugu na machafuko" yaliyoshuhudiwa hapo jana baada ya maandamano ya kupinga mapendekezo ya serikali yake ya kupandisha kodi na ushuru kugeuka kuwa ya vurugu huku akilaani uvamizi wa Bunge.

"Cha kusikitisha zaidi, shambulio la leo (jana) dhidi ya utaratibu wa Katiba ya Kenya limesababisha watu kupoteza maisha, pia uharibifu wa mali, unajisi wa taasisi na nembo za uhuru wetu. Matukio ya leo yanaashiria mabadiliko muhimu ya jinsi tunavyoshughulikia vitisho kwa usalama wa taifa letu. Nalihakikishia taifa kuwa serikali imekusanya rasilimali zote ilizokuwa nazo ili kuhakikisha kuwa matukio ya aina hii hayatajirudia tena na kwa gharama yoyote ile."

Rais Ruto amewaambia waandishi habari kuwa serikali yake itatoa jibu kamili na mwafaka wa haraka kwa matukio ya uhaini akisema maandamano hayo yalivamiwa  na watu hatari.