6 wapitishwa mchuano urais TLS, wamo Mwabukusi, Kapt. Bendera

By Restuta James , Nipashe
Published at 10:07 AM Jun 26 2024
Mwanaharakati wa haki za binadamu, Boniface Mwabukusi.
Picha: Maktaba
Mwanaharakati wa haki za binadamu, Boniface Mwabukusi.

MAWAKILI sita, akiwamo mwanaharakati wa haki za binadamu, Boniface Mwabukusi, wameteuliwa kuwania kiti cha urais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Taarifa ya TLS kwa umma inataja mawakili sita walioteuliwa kuwania urais, orodha hiyo ikiwa na jina la Mwabukusi, akichuana na Wakili Kapteni Ibrahim Bendera, aliyebobea katika sheria zinazohusu bahari.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa, walioteuliwa kuwania urais mbali na Mwabukusi anayetoka mkoani Mbeya na Kapteni Bendera anayetoka Ilala, ni Emmanuel Muga (Ilala), Revocatus Kuuli (Mzizima), Paul Kaunda (Kanda ya Magharibi), Sweetbert Nkuba (Kinondoni).

MWABUKUSI

Ni mwanaharakati wa haki za binadamu, utawala bora na haki ardhi. Ndiye aliyefungua kesi dhidi ya serikali kupinga makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya DP World kuendesha Bandari ya Dar es Salaam.

KAPTENI BENDERA

Huyu ni wakili mbobevu katika sheria zinazohusu bahari. Anakumbukwa zaidi katika kesi ya watuhumiwa wa meli ya uvuvi ya Tawariq 1, maarufu Samaki wa Magufuli, iliyokamatwa nchini Machi 2009.

Katika kesi hiyo, Kapteni Bendera alishinda serikali na wateja wake kudai fidia ya meli iliyokuwa na thamani ya Dola za Marekani 2,300,000 (uthamini wa mwaka 2008) pamoja na Sh. 2,074,249,000 ambazo ni gharama za tani 296.3 za samaki.

Ana Shahada ya Uzamili katika Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akisomea Sheria za Bahari na Kazi. Pia ana Shahada ya Kwanza ya Sheria) kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

REVOCATUS KUULI

Huyu amebobea katika sheria za kiraia na jinai, za kimataifa, haki za binadamu, upatanishi, usuluhishi na masuala ya katiba.

NKUBA

Wakili Sweetbert Nkuba amebobea katika kesi za madai, akitumia maendeleo ya kiteknolojia kuwafikishia wananchi huduma za kisheria. Ndiye mwanzilishi wa WakiliApp ambayo ni akili bandia ya kutoa msaada wa kisheria.

PAUL KAUNDA

Wakili huyu ni mbobevu wa sheria za bima, biashara na ufilisi. 

Mbali na kiti cha urais, taarifa ya TLS ina jina la Laetitia Ntagazwa (Iringa), aliyeteuliwa kuwania nafasi ya makamu wa rais.

Inaelezwa katika taarifa hiyo kuwa Aziza Msahi (Ilala), hakustahili kuchaguliwa kwa mujibu wa kifungu cha 15 (3)(d) cha Sheria ya Chama cha Wanasheria Tanganyika, Sura 307, kama ilivyorekebishwa na Sheria ya Sekta (Marekebisho Mengineyo) Na. 11 ya 2023.

Vifungu hivyo vinambana wakili huyo kwa kuwa haendeshi au kusimamia kampuni ya mawakili yenye wafanyakazi watano au zaidi wanaohudumu katika bodi yoyote ya uongozi inayotambuliwa.

Katika nafasi ya mweka hazina, aliyeteuliwa ni Stella Rweikiza (Kinondoni), wakati wa nafasi ya Mwenyekiti Chama cha Wanasheria Vijana (AYL) walioteuliwa ni Emmanuel Ukashu (Ilala), Denis Eliasaph (Kinondoni), huku Victor Kweka (Dodoma), Joseph Lameck na Moses Misiwa (Mwanza) wakikosa sifa kwa mujibu wa kanuni mbalimbali za chama hicho.

Kutangazwa majina hayo kunatoa nafasi ya wateuliwa kuanza kampeni Jumamosi ya Julai 6 hadi Agosti Mosi mwaka huu na uchaguzi ukitarajiwa kufanyika Agosti 2, mwaka huu jijini Dodoma.