MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Babati (BAWASA) mkoani Manyara imekusanya Sh. milioni 12 kwa kutoza faini watu waliunganisha maji kinyemela.
Mamlaka hiyo ilibaini watu hao kujihusisha na vitendo hivyo na kuiba maji kinyume cha sheria kati ya Januari mwaka juzi na Januari mwaka jana.
Meneja Huduma kwa Wateja wa BAWASA, Rashid Charahani, alisema fedha hizo walizokusanya zimetumika kuboresha miundombinu ya maji na kununua pikipiki za mafundi ili kuboresha huduma kwa wananchi.
Charahani, alisema kwa kipindi hicho matukio zaidi ya 20 ya uharibifu wa miundombinu ya maji yaliripotiwa na hatua kuchukuliwa kwa wahusika.
Alisema wanapobaini mtu ameharibu miundombinu ya maji, anatozwa faini kuanzia Sh. 500,000 mpaka Sh. milioni 50 au kifungo cha miezi 12 au vyote kwa pamoja.
Kwa mujibu wa Charahani, ili kuhakikisha wizi wa maji unakomeshwa, BAWASA inatoa motisha ya Sh. 200,000 kwa mtu anayetoa taarifa hizo na za uharibifu wa miundombinu na mtoa taarifa kulindwa.
"Ofa hiyo (motisha), mtu akitoa taarifa za wizi wa maji kama ni za kweli na tukijiridhisha tunaanza kumuandalia malipo yake anayapata ndani ya siku saba na hii ni kwa wote hata watumishi wetu wote wanalipwa shilingi 200,000," alisema.
Aliyataja maeneo yaliyokithiri kwa wizi wa maji kuwa ni Katesh Mjini, Babati na Magugu.
Mkazi wa Mtaa wa Maisaka A, Adela Godwin, aliwataka BAWASA kuongeza nguvu kukagua wanaolima bustani kwa kuwa baadhi yao wanahujumu miundombinu ya maji na kuiba maji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED