Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mkoani Singida limepitisha rasimu ya mpango wa bajeti ya Sh. bilioni 33.955 kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo, Abdallah Karoboneka, akiwasilisha leo taarifa ya rasimu ya mpango huo katika kikao cha Baraza la Madiwani, amesema kati ya fedha hizo, Sh bilioni 4 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huku sehemu iliyobaki ikielekezwa kwenye mishahara ya watumishi na matumizi mengine ya kawaida.
Karoboneka amesema kuwa baadhi ya miradi ya maendeleo iliyopangwa kutekelezwa kupitia bajeti hiyo ni pamoja na ukamilishaji wa Kituo cha Afya Ilunda, ujenzi wa vyumba vya madarasa 40 katika Shule ya Sekondari Mwangeza, pamoja na kuboresha stendi za Iguguno na Nduguti.
Aidha, amesema halmashauri inapanga kukamilisha ujenzi wa zahanati tatu katika maeneo ya Mwando, Mazangili na Isene ili kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Akizungumza katika kikao hicho, Mbunge wa Iramba Mashariki, Jesca Kishoa, aliitaka halmashauri kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuongeza uwezo wa kugharamia miradi ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED