AIRTEL Tanzania imeingia ubia wa miaka mitatu na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), kwa lengo la kuongeza tija katika sekta ya kilimo kwa njia ya kidigitali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wakulima na wajasiriamali nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano hayo, leo mkoani Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania Dinesh Balsingh, amesema ushirikiano huo ni moja kati ya juhudi za Airtel Tanzania kuunga mkono serikali katika kuleta matokeo chanya katika maisha ya Watanzania.
"Hii ni kwakua tunaamini wakulima wanastahili kuwa miongoni mwa vikundi vinavyotakiwa kunufaika na ukuaji wa teknolojia nchini. Hivyo, Ushirikiano wetu na TADB unalenga katika kutatua changamoto zinazowakabili wakulima kwa kutumia bidhaa mbalimbali za kidijitali ambazo zitaibua masoko mapya kwa wakulima mijini na vijijini.
"Bidhaa hizo zitawezesha uzalishaji wa wakulima na kuongeza mapato yao. Na hii ni kutokana na jinsi kilimo kilivyo muhimu katika kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi kwa kuwa zaidi ya asilimia 70 ya watu wamejiajiri katika sekta hiyo," amesema Balsingh.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TADB, Frank Nyabundege, amebainisha kuwa ushirikiano huo una dhamira ya kufanikisha kupanua ushirikiano wa sekta ya kifedha kwa wadau mbalimbali ndani ya sekta ya kilimo, wakiwemo wakulima, wajasiriamali wadogo vijijini, hasa wanawake na vijana.
"Ushirikiano wa Airtel na TADB utafungua milango ya fursa katika sekta ya kilimo na utatoa uwanja mpana kwa wakulima kujipatia masuluhisho kwenye mahitaji na changamoto wanazokutana nazo katika shughuli zao za kila siku. Pia ni mwanzo wa mabadiliko makubwa yatakayowagusa wakulima wote nchini Tanzania," amesema Nyabundege.
Ameongeza kuwa ushirikiano huo unakwenda sambamba na mikakati ya serikali ya kuunga mkono juhudi za wadau wa kilimo kwa kupambana na changamoto mbalimbali ndani ya sekta ya kilimo kwa kuwawezesha wakulima kifedha kama ilivyotajwa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa mkutano wa wadau wa COP28 mwaka 2023.
"Tunatakiwa kubadilika na kufanya kilimo endelevu kwa kuunga mkono ubunifu mbalimbali unaoendana na hali ya sasa," amesema Nyabundege.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED