ACT walia magari ya serikali kutafuna mabilioni ya bajeti

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:53 AM Jul 26 2024
Kiongozi wa Chama hicho, Dorothy Semu
Picha: Mtandao
Kiongozi wa Chama hicho, Dorothy Semu

CHAMA cha ACT Wazalendo kimesema matumizi ya serikali, hasa katika ununuzi wa magari na kugharamia mafuta na matengenezo yake, vinaongeza ugumu wa maisha kwa wananchi.

Viongozi wakuu wa chama hicho wamesema wanaumia kuona wakati wananchi wakiteswa na umaskini mijini na vijijini na kujifunga mikanda kiuchumi kukabiliana na kupanda kwa bei za bidhaa na huduma, serikali imeendelea na matumizi yasiyo na tija huku ukaguzi ukibaini kuwapo upigaji fedha za umma. 

Walilalamikia hayo jana katika mikutano ya hadhara iliyofanyika mikoa ya Simiyu, Dodoma, Kigoma na Ruvuma. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa na Wizara ya Fedha bungeni mwaka 2022, serikali ilikuwa na magari 15,742, pikipiki 14,047 na mitambo 373 huku ikitumia zaidi ya Sh. bilioni 500 kila mwaka kwa ajili ya ununuzi wa magari mapya, mafuta, vipuri na matengenezo.

Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba aliarifu Bunge kuwa serikali ina mpango wa kupunguza matumizi katika eneo hilo kwa kuwakopesha fedha za kununua magari watumishi wa umma badala ya kutumia magari ya serikali. 

Kiongozi wa Chama hicho, Dorothy Semu, akiwa wilayani Bahi, mkoani Dodoma jana alisema, "Tunashuhudia ubadhirifu na upotevu mkubwa wa fedha unaofanywa na watendaji wa serikali. Mwaka huu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG - ripoti ya 2022/23) ameonesha fedha zilizo hatarini kupotea kutokana na vitendo vya ubadhirifu ni Sh. trilioni 3.4. 

"Hakuna aliyewajibishwa. Wakati huohuo viongozi wanaendelea kufanya matumizi ya anasa kwa kujinunulia magari ya kifahari, kujiongezea posho, safari za nje na mishahara. Kwenye bajeti ya mwaka huu, katika kila Sh. 1,000 itakayokusanywa wamejipangia Sh. 700 ni kwa matumizi yao." 

Doroth alilalamika kuwa serikali inatumia fedha nyingi kununua mafuta ya petroli na diseli kwa ajili ya magari yake, akisisitiza kuwa upo uwezekano wa kupunguza matumizi hayo kwa kutumia nishati ya gesi asilia iliyopo nchini. 

Alisema gesi asilia ingelisaidia taifa kupunguza nauli za mabasi na usafiri na kuongeza ajira, hivyo kupunguza ugumu wa maisha kwa wananchi.

Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Tanzania Bara, Isihaka Mchinjita, akiwa Peramiho, mkoani Ruvuma jana, alisema ubadhirifu unaongeza mzigo kwa wananchi. Fedha zinazotengwa haziendi kushughulikia matatizo ya msingi ya wananchi. Ndio maana serikali imekuwa na madeni makubwa. 

"Wote tunaona hali ilivyokuwa ngumu. Ninataka niwaambie wana Peramiho na Watanzania 
 wote, ACT Wazalendo tumedhamiria kuifikisha mwisho hali hii. Wajibu wenu ni kuikataa CCM na kuichagua ACT Wazalendo. 

"Tutahakikisha tunaondosha hali hii kwa kuilinda kila senti ya fedha zenu zinazokusanywa kutokana na jasho lenu inatumika kujenga taifa la wote kwa maslahi ya wote," alisema Makamu Mwenyekiti. 

Ado Shaibu, Katibu Mkuu wa chama hicho, akiwa Busega, mkoani Simiyu jana, alisema ugumu wa maisha umeongezwa na ukopaji wa serikali, akisisitiza kuwa athari kubwa za ukopaji holela zinaangukia kwenye mabega ya wananchi walalahoi. 

"Wananchi wanaongezewa kodi, ushuru na makato katika huduma muhimu kama vile ushuru kwenye mazao ya kilimo ili kulipa madeni haya.

"Wakulima, wachimbaji wadogo, wafanyabisahara na wafanyakazi wote wanalia utitiri wa kodi, ushuru na tozo. Serikali inawakamua wananchi wake kulipa madeni ambayo hawakunufaika nayo.

"Serikali inatumia sehemu kubwa ya fedha zetu kwenda kuhudumia deni badala ya kutoa huduma kwa wananchi walio wengi. Kila Sh. 1,000 tutayokusanya, Sh. 370 inakwenda kulipa deni," alisema.

Kiongozi mstaafu wa chama hicho, Zitto Kabwe, akiwa Jimbo la Kigoma Kaskazini, alisema sera alizodai "mbovu" za uchumi wa nchi zimesababisha serikali kushindwa kuongeza tija katika kilimo, uwekezaji na matumizi ya rasilimali za nchi kuondoa umaskini.

"Kwa sasa gharama za maisha ni tatizo kuu kwa Watanzania, wananchi wamechoshwa na umaskini wanataka mabadiko. Tunaelewa mzigo wa gharama kubwa za maisha na tunaahidi kuanzisha sera zinazodhibiti mfumuko wa bei na kupunguza bei za bidhaa na huduma muhimu," alisema.

Viongozi wakuu wa ACT Wazalendo wanaendelea na ziara ya kuzunguka majimbo yote Tanzania Bara, awamu ya kwanza ikihusisha majimbo 125. 

Jana walikuwa majimbo ya Bahi, Maswa, Itilima, Kigoma Kaskazini na Peramiho. Na leo wataendelea na ziara katika majimbo ya Buhigwe, Rorya, Tarime Mjini, Manyoni, Buyungu na Songea Mjini.