Simba yaibomoa Mashujaa

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 09:16 AM Jun 23 2024
news
Picha: Mtandao
Omari Omari.

HUKU ikiwa katika mchakato wa kusaka beki mpya wa kati ili kurithi mikoba ya Mkongomani Henock Inonga, Simba inatajwa imekaribia kumsajili mshambuliaji wa Mashujaa FC, Omari Omari, taarifa za ndani zimeeleza.

Inonga, alikuwa na mkataba na Simba hadi Juni, mwakani, anatajwa kujiunga na FAR Rabat ya Morocco.

Tayari Simba imemtangaza beki wa kati kutoka Coastal Union, Lameck Lawi, ambaye anaziba pengo la Kennedy Juma, timu hiyo bado haijapata mbadala wa Inonga ambaye hatakuwa sehemu ya kikosi chao katika msimu mpya.

Taarifa za ndani za Simba zinadai klabu hiyo iko katika  mazungumzo na beki wa kati wa Asec Mimosas ya Ivory Coast, Anthony Tra Bi Tra.

"Naweza kukwambia muda wowote tunaweza kukamilisha dili hilo na kumtangaza, ni mchezaji mzuri, yeye na Adam Adam, waliisaidia sana Mashujaa kubaki Ligi Kuu baada ya kusajiliwa kipindi cha dirisha dogo la usajili," alisema mtoa taarifa.

Mbali na mchezaji hiyo, Simba pia inapambana kuhakikisha inapata saini ya beki wa kushoto wa KMC, Rahim Shomari, ili kuja kusaidiana na Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr.'

Chanzo hicho kimesema Rahim ambaye makuzi yake yalianzia katika kikosi cha vijana cha Simba, anatajwa kurejea nyumbani na KMC imesema itakuwa tayari kumruhusu kuondoka itakapolipwa Sh. milioni 100.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, aliliambia gazeti hili bado wako katika mazungumzo na beki mwingine kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kucheza katika nafasi ya ulinzi.

Ahmed alisema wanajipanga kuwa na mabeki wanne watakaocheza katika nafasi hiyo na wanaamini watakuwa ni wazoefu na wenye ubora mkubwa.

"Bado tunahitaji beki mwingine, tunahitaji watu wa kazi kweli kweli, tumempata Lameck Lawi, tunaye Fondoh Che Malone, pia yupo kijana, Hussein Kazi, sasa tunahitaji mlinzi mwingine wa kimataifa ili wawe wanne kwa lengo la kuimarisha ulinzi zaidi msimu ujao," alisema Ahmed.

Alisema lengo la kumsajili Lawi, ni kuifanya timu hiyo ipunguze idadi ya mabao ya kufungwa kwa sababu msimu uliopita iliruhusu magoli mengi kwa mara ya kwanza baada ya misimu kadhaa kupita.

"Kuondoka kwa Kennedy, kunafungua milango ya kijana mwingine wa Kitanzania kutoka Coastal Union anayeitwa Lawi kuonekana, tuko katika mipango ya kuitengeneza Simba imara na thabiti, kumbuka msimu uliomalizika Simba imeruhusu mabao mengi sana, kulikuwa 'kunavuja' sasa huyo na mwingine atakayetua, wanakuja kuziba eneo hilo ili irudi ile Simba inayoruhusu mabao machache, " alisema.