KLABU ya Simba imetajwa iko katika mazungumzo wa beki wa kati ya RS Berlane, Issouf Dayo, ambaye ni raia wa Burkina Faso, ili kumsajili kipindi cha dirisha dogo, kwa lengo la kuongeza nguvu kwenye kikosi chake.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya Simba zinasema baada ya kumalizana na Elie Mpanzu, benchi la ufundi, likiongozwa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids, limewaeleza viongozi wanahitaji kujiimarisha zaidi, ili kufanya vyema katika hatua ya makundi ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Chanzo hicho kilisema Fadlu aliweka wazi anahitaji beki ambaye ni mrefu, mwenye nguvu na uzoefu wa michuano hiyo inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
"Kwa sasa viongozi wetu wanaendelea na mazungumzo na menejimenti ya beki huyo, ili kupata saini yake, nafikiri itakuwa rahisi kidogo kwa sababu mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu, hivyo uhamisho wake hautagharimu ada kubwa sana," kilisema chanzo chetu.
Kiliongeza mlinzi huyo mwenye umri wa miaka 33 na mrefu futi sita na inchi mbili, ameonekana kumvutia Fadlu ambaye anahitaji awe na beki wa aina hiyo katika kikosi chake.
"Tuna walinzi lakini hatuna walinzi katili, ambao wanaweza kuwatisha mafowadi kwa umbile na hata uchezaji wa kutumia akili na nguvu pia. Tuna walinzi wazuri sana, lakini wote ukiwaangalia ni wale ambao wanatumia zaidi akili, linapokuja suala la nguvu zaidi inakuwa tatizo, nadhani atakuja kuwa suluhisho kwa mastraika wakorofi, wenye nguvu na wajanja na akina Mabululu (Cristovao Paciencia).
Kocha (Fadlu), amewaambia viongozi ana mabeki wazuri, lakini pia anahitaji aina hiyo ya beki, ambaye hapishani na mtu, kama ilivyokuwa kwa Joash Onyango kipindi chake yupo kwenye fomu, lakini huyu uwezo wake ni mara nyingi zaidi yake, kucheza RS Berkane siyo mchezo," kiliocheza chanzo chetu.
Wakati viongozi wakiwa katika mchakato wa kumwania beki huyo, inaelezwa huenda wakampoteza kipa, Ayoub Lakred, raia Morocco, anayetakiwa na Wydad Casablanca ya nchini kwao.
Taarifa zinasema nyota huyo wa zamani wa AS FAR Rabat, alisaini mkataba wa mwaka mmoja na Simba na ikifika dirisha dogo la usajili atakuwa amemaliza nusu ya mkataba wake.
Habari zinasema vigogo hao wa Morocco, wanamhitaji kwenda kusaidiana na kipa, Yusuf El Motie.
Hata hivyo, inaweza kuwa ni rahisi zaidi kwa Simba kuachana na kipa huyo, kwa sababu hajaonekana dimbani tangu kuanza kwa msimu kutokana na majeraha yaliyokuwa yanamkabili.
Kipa huyo aliondolewa kwenye mfumo wa usajili ya kimataifa TMS, nafasi yake ikachukuliwa na straika, Leonel Ateba, huku mwenyewe akiendelea kulipwa stahiki zake kama kawaida.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kwa sasa hawezi kuzungumzia chochote kuhusu usajili wa dirisha dogo, kwa sababu wakati wake bado, badala yake anawaomba wanachama na mashabiki, macho yao wayaelekeze kwenye mchezo wa dabi utakaofanyika Oktoba 19, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
"Tupo katika kipindi cha hamasa cha mchezo wetu dhidi ya Yanga, kwa sasa tuache kwanza, ila muda utafika, Desemba haipo mbali, kila kitu kitajulikana," alisema Ahmed.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED