Simba kamili kuivaa CS Constantine

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 10:04 AM Dec 08 2024
Simba kamili kuivaa CS Constantine.
Picha: Mtandao
Simba kamili kuivaa CS Constantine.

KIKOSI cha Simba leo saa 1:00 usiku kwa saa za Tanzania, kitashuka kwenye Uwanja wa Mohamed Hamlaoui kwenye mji wa Constantine nchini Algeria, kucheza dhidi ya CS Constantine katika mchezo wa raundi ya pili Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi, huku Kocha Mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids, amesema watacheza mchezo huo kimkakati, huku wapinzani wao wakilia kuwakosa wachezaji watatu muhimu.

Katika mchezo huo wa Kundi A, timu zote zitaingia uwanjani zikiwa na kumbukumbu ya kushinda mechi zao za raundi ya kwanza, Simba ikishinda nyumbani bao 1-0 dhidi ya Bravo do Maquis ya Angola na CS Constantine ikishinda bao 1-0 dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia.

Timu yoyote itakayoshinda mchezo wa leo itakaa juu ya kilele cha msimamo wa kundi hilo.

Kocha Fadlu amesema maandalizi ya mchezo huo yamekamilika, ikiwemo kuwasoma wapinzani wake, jinsi wanavyocheza na wachezaji wao bora na hatari na amewaelekeza wachezaji wake jinsi gani ya kukabiliana nao.

"Mandalizi yamekamilika, nimefurahi kuja kwa golikipa Hussein Abel ili kuongeza idadi yao kama lolote likitokea, natarajia mechi itakuwa ngumu na ya kasi sana, tumejiandaa kwa hilo, nimewaona wana mabeki wazuri, lakini katika mchezo huu ni muhimu kwetu kupata bao ili kutuweka mchezoni," alisema.

Fadlu, raia wa Afrika Kusini, alisema katika mechi ya leo, wachezaji wake wanatakiwa kuwa na kasi wakati wanashambulia, lakini wanaponyang'anywa mpira amewaelekeza kuwa na nidhamu ya kurudi nyuma haraka ili kusaidia ulinzi.

"Tunatakiwa kucheza mechi hii kimkakati, siyo ili mradi tunacheza, kwa sababu tuna machaguo mawili, kushinda au kutoa sare, hivyo hatutakiwi kufunguka sana, ila tunapokuwa na mpira tunatakiwa tuwe na kasi na maamuzi ya haraka," alisema Fadlu.

Kocha Mkuu wa CS Constantine, Kheireddine Madoui, ameonekana kuhuzunika kuwakosa wachezaji wake watatu muhimu katika mchezo wa leo.

Wachezaji hao ni kiungo mshambuliaji, Abdennour Iheb Belhocini mwenye mabao mawili na asisti' moja katika michezo 10,  kiungo mkabaji Salifou Tapsoba aliyetumika katika michezo sita ya timu hiyo na straika, Mounder Temine.

“Tamine na Belhoussini hatutakuwa nao kutokana na majeraha, Tapsoba ameondoka kwa ajili ya majukumu ya kimataifa, tunapokosa wachezaji muhimu tunajua kuwa tutakutana na changamoto kubwa. Hii ni hali inayotufanya tuwe na wasiwasi," alisema Madoui

Hata hivyo, alisema anatarajia wachezaji waliopo watapambana kwa nguvu kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

"Simba ni timu inayoheshimiwa sana katika mashindano ya kimataifa kutokana na uzoefu wake, tunahitaji kujiandaa kwa umakini, tunajua kuwa mchezo huu ni muhimu sana kwetu kwa sababu pointi zake zitakuwa na maana kubwa katika safari yetu ya kufika mbali katika michuano hii," alisema kocha huyo.