Harry Kane mwingereza wa kwanza kufunga mabao 500

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 02:31 PM Feb 15 2026
Harry Kane
Picha: Mtandao
Harry Kane

Harry Kane ameweka historia ya kuwa mchezaji wa kwanza wa soka mwingereza kufikisha mabao 500 katika kipindi chake cha uchezaji kwenye michezo rasmi.

Mshambuliaji huyo wa Bayern Munich alifikia hatua hiyo kwa kufunga mabao mawili dhidi ya Werder Bremen kwenye Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga, Jumamosi.

Kane tayari Desemba mwaka jana aliweka rekodi ya kuwa mwingereza aliyefunga mabao mengi zaidi, akimpiku Jimmy Greaves aliyekuwa anashikiria rekodi ya kufunga mabao 474.

Umekuwa msimu mwingine wa kuvutia kwa Kane, ambaye ana mabao 26 katika michezo 22 ya Bundesliga.

Bao la kwanza la Kane katika soka la kulipwa ilikuja miaka 15 iliyopita alipofunga akiwa na umri wa miaka 17 akiichezea Leyton Orient dhidi ya Sheffield Wednesday, kabla ya kufunga mawili kwa Leicester, tisa kwa Millwall, 280 kwa Tottenham Hotspur na kwa sasa ana mabao 126 kwa Bayern Munich.

Kane pia ndiye mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi kwa kikosi cha timu ya taifa ya England akiwa na 78.

Karibu nusu ya mabao yake yamepatikana katika Ligi Kuu England (213).

Baada ya hapo amefunga mabao 89 kwenye Bundesliga.

Kane alikuwa tayari mwingereza aliyefunga mabao mengi zaidi katika mashindano ya klabu barani Ulaya, kwani kwa sasa ana mabao 48, 18 zaidi ya Wayne Rooney, ambaye anashika nafasi ya pili kwenye orodha hiyo.

Rekodi ya Greaves kama mwingereza aliyefunga mabao mengi zaidi ilidumu kwa kipindi cha miaka 60, hadi Kane alipofikisha idadi yake ya mabao miezi miwili iliyopita.

Kane aliondoka Ligi Kuu England akiwa mfungaji bora wa pili kwa mabao mengi katika mashindano hayo, huku Alan Shearer akishikilia rekodi hiyo akiwa na mabao 260.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za Soka (IFFHS), Shearer anashika nafasi ya nne katika orodha ya wafungaji wa muda wote wa Uingereza akiwa na mabao 409, huku Steve Bloomer - ambaye alicheza mwanzoni mwa karne ya 20 - akiwa wa tatu akiwa na mabao 412, nyuma ya Greaves na Kane.

Dixie Dean anashika nafasi ya tano akiwa na mabao 396 na Rooney anashika nafasi ya sita akiwa na mabao 360.

CHANZO: ESPN