Gamondi awaita nyota mawindoni

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 01:03 PM Jun 30 2024
 Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi.
Picha: Maktaba
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi.

MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara wanatarajia kuingia kambini kesho kwa ajili ya kuanza mazoezi kuelekea msimu mpya wa mashindano wa mwaka 2024/2025.

Wito huo umetolewa na Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, ambaye bado yuko kwao alikokwenda kwa ajili ya mapumziko baada ya kumaliza msimu uliopita.

Taarifa kutoka Yanga zinasema Gamondi amewataka wachezaji wote wapya na wale waliosalia katika kikosi hicho kuwapo jijini Dar es Salaam Julai Mosi tayari kuanza kambi.

Chanzo hicho kimesema Gamondi ametuma ujumbe wa simu kwa viongozi, kuhakikisha wanamaliza mchakato wa usajili haraka huku akiwataka wachezaji wote kuripoti kambini kuanzia Julai Mosi, mwaka huu ili kuanza mawindo.

"Kocha ametuma ujumbe, amesema bila kujali mchezaji mpya au wa zamani, pamoja na watu wa benchi la ufundi kila mmoja anatakiwa awe amewasili kambini Julai Mosi, kwa hiyo viongozi wameambiwa wamalize kila kitu kuhusu usajili ili akifika isiwe tena kuna mchezaji hajafika au kukamilisha usajili," kimesema chanzo chetu.

Naye Rais wa Yanga, Hersi Said, amesema klabu hiyo itaanza kutangaza nyota wapya waliosajiliwa na inaowatema kuanzia kesho.

Hersi amesema usajili wa kikosi chao umeshakamilika na kinachosubiriwa ni kukabidhi majina katika Idara ya Habari ya klabu hiyo.

"Tumeshasajili karibu asilima 99, kazi imekwisha, hivi sasa tumeiachia tu Idara ya Habari kutengeneza njia nzuri ya kutambulisha wachezaji, kuna maeneo ambayo tumelazimika kuyaboresha katika  kikosi chetu ili kuwa bora zaidi, kwa hiyo nichukue fursa hii kuwaambia Wana-Yanga wawe tayari kuanzia tarehe moja tutaanza kutoa taarifa za usajili, wachezaji wetu wapya na wale tunaowaongezea mikataba na tutakaowaacha," Hersi amesema.

Yanga inatarajia kuweka kambi yake Ulaya lakini imeweka wazi imepokea mwaliko wa kucheza mechi za kirafiki za kimataifa katika nchi za Kenya na Afrika Kusini.

Mabingwa hao pia walitangaza watacheza dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika kilele cha Siku ya Mwananchi.

Klabu hiyo pia imefanikiwa kuwabakisha nyota wake nyota waliokuwa wanatakiwa na klabu za nje ya Tanzania akiwamo Stephane Aziz Ki, Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua na Djigui Diarra.