Baada ya kupoteza mechi ya kwanza ya hatua ya makundi usiku wa kuamkia leo, Yanga imetamba itafuzu kucheza robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kishindo ikiwa nyumbani.
Wenyeji AS FAR walijibu mapigo kwa kuifunga Yanga bao 1-0 ambapo Waarabu hao wa Morocco sasa wamefikisha pointi nane.
Msemaji wa Yanga, Ali Kamwe, ameiambia Nipashe Digital hawana hofu na sasa nguvu zao wanazielekeza katika mechi ya mwisho itakayochezwa wiki ijayo kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
“Hii imeshaisha, naomba niseme Yanga itaenda kufuzu kwa kishindo pale Guantanamo Bay, hili sio jambo la kushangaza, tutashinda mabao mengi, tutafuzu,” Kamwe alisisitiza.
Yanga imebakia na pointi tano huku vinara wa Kundi B, Al Ahly ya Misri wenye pointi tisa wameshafuzu hatua inayofuata. Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara watamaliza hatua ya makundi kwa kuwakaribisha JS Kabylie kutoka Algeria ambayo inakuja kukamilisha ratiba kutokana na kuburuza mkia katika kundi lao.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED