Tenisi taifa waenda Botswana

By Shufaa Lyimo , Nipashe Jumapili
Published at 04:17 PM Jul 14 2024
TIMU ya Taifa ya mchezo wa tenisi.
Picha: Shufaa Lyimo
TIMU ya Taifa ya mchezo wa tenisi.

TIMU ya Taifa ya mchezo wa tenisi imeondoka jana asubuhi kuelekea Botswana kushiriki mashindano ya Dunia kanda ya tano yatakayoanza kesho mpaka Julai 20.

Akizungumza na Nipashe jana muda mfupi kabla ya timu hiyo haijaondoka, Makamu wa Rais wa Chama cha mchezo wa tenisi Tanzania (TAA), Rajabu Borri, alisema timu hiyo imeondoka na wachezaji wanne.

"Kwa sasa tunajiandaa kuelekea Botswana, tumelazimika kuwahi ili wachezaji wakazoee hali ya hewa pamoja na mazingira ya mchezo, alisema Borri.

Alisema kwa upande wao kama chama kwa kushirikiana na Serikali wameiandaa timu hiyo vizuri ili kuhakikisha inakwenda kuiwakilisha vema Tanzania. 

Aidha, alisema mashindano hayo yatakuwa na ushindani mkubwa kwa kuwa yatashirikisha timu kutoka Mataifa mbali mbali hivyo amewataka wachezaji kucheza kwa tahadhari kubwa. 

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Salum Mvita alisema hana wasiwasi na wachezaji wake kwani amewapa mbinu ambazo zitawasaidia kupata matokeo mazuri. 

"Tumefanya maandalizi kwa kipindi kirefu kwa ajili ya kuipa heshima nchi yetu kupitia mashindano haya, tunaomba watanzania watuombee tutimize malengo yetu, alisema Mvita.