BAADA ya kufanyika kwa pambano la ngumi la 'Fight for Change' wiki iliyopita waandaaji wametimiza ahadi kwa kutoa msaada kwa kituo cha kulelea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu cha Malaika, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, muandaaji wa pambano hilo ambaye pia ni bondia, Karim Bhaloo, amesema wametimiza ahadi waliyoitoa kabla ya pambano hilo kwa kutoa msaada huo.
"'Figt for Change' ina lenga kusaidia zaidi jamii, tulipanga kutoa msaada huu na leo tumetimiza, tutakuwa tukifanya hivi kila tunapoandaa pambano," alisema Bhaloo.
Alisema msaada walioutoa ni pamoja na vyakula, mafuta ya kupika, sabuni, sukari, mitungi ya gesi na bidhaa nyinginezo.
Aidha, mmoja wadhamini wa pambano hilo, Abdulrahim Noray ambaye ni mkurugenzi w akampuni ya Oscon Builders, alisema wataendelea kudhamini kuunga mkono juhudi za waandaaji wapambano hilo katika kusaidia jamii.
"Nifahari kwetu kuona wanamichezo wanakumbuka jamii, msaada huu ni chachu kwa mabondia na wanamichezo wengine kuwasaidia watanzania wenzetu pale wanapopata nafasi kama walivyofanya hawa wenzetu," alisema Noray.
Kwa upande wake, mlezi wa kituo hicho, Neema Mohamed, alishukuru kwa msaada huo na kutoa wito kwa watu wengine kuwasaidia kwa kuwa watoto wanaolelewa katika kituo hicho wana uhitaji mkubwa.
"Kituo hiki cha Kinondoni kuna watoto 32 ambao wapo wanafunzi kuanzia chekechea mpaka wengine ngazi ya vyuo, uhitaji ni mkubwa sana kwenye eneo la elimu na afya, tuwaombe watanzania wenzetu kuendelea kutusaidia," alisema Neema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED