NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, ameiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kushirikiana na Kampuni ya Kili International Marathon, waandaji wa mbio za Kili Marathon, kuhakikisha mbio hizo zinatumika kutangaza vivutio vya utalii nchini.
Dk. Biteko ametoa agizo hilo leo, Februari 23, 2025 mkoani Kilimanjaro, wakati aliposhiriki mbio za Kili Marathon za kilomita tano.
“Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, iangalie namna bora ya kushirikiana na Kili Marathon, ili mbio hizi ziwe nyenzo ya kutangaza utalii wetu na kuwa fursa kwa wageni kutembelea vivutio vyetu vya utalii,” amesema Dk. Biteko.
Amesema mbio hizo zimeendelea kuwavutia watu wengi zaidi ndani na nje ya nchi, na mwaka huu zaidi ya watu 20,000 wameshiriki mbio hizo.
Pamoja na hayo, Dk. Biteko ametoa rai kwa Watanzania kushiriki mashindano hayo, kwa vile yana fursa mbalimbali ikiwamo biashara, pamoja na kuzingatia ulaji wenye afya na kufanya mazoezi kuepuka magonjwa yasiyoambukiza.
Katika hatua nyingine, amesema mbio hizo ziwe kichocheo cha kudumisha amani na umoja miongoni Watanzania huku akiwashukuru washiriki wa mbio hizo kutoka nje ya nchi.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi. amesema kuwa Kili Marathon ni mbio zilizoonesha mfano na Wizara yake itaendelea kushirikiana nao. ili kuzikuza zaidi.
Ameendelea kusema wizara kwa kushirikiana na wadau, itaandaa mazingira mazuri kwa vijana na wanamichezo wote, kwa kuboresha miundombinu, kwa ajili ya michezo mbalimbali nchini na kutoa fursa ya kufanya mazoezi na kushindana kimataifa.
Pia, amewapongeza washindi wote wa mbio hizo, sambamba na kulielekeza Baraza la Michezo Tanzania (BMT), kuandaa mpango mkakati, kwa ajili ya mchezo wa riadha, ili nchi iweze kupata wanariadha mahiri watakaoiwakilisha nchi kimataifa.
Aidha, washindi wa Kili Marathon wa viwango mbalimbali vya mbio walitunukiwa zawadi za fedha na medali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED