WAKAZI 189,936 wa halmashauri ya Ushetu, mkoani Shinyanga, wanatarajia kunufaika na mradi wa maji wa Ziwa Victoria na kuondokana na magonjwa ya mlipuko ya kuhara na homa ya matumbo.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika Oktoba, mwakani 2026. Unatekelezwa na Mkandarasi Sihotech Engineering Co. Ltd ya jijini Dar es Salaam, kwa kushirikiana na Kampuni ya Mpole Construction and Co. Ltd ya Iringi.
Utagharimu Sh. bilioni 44 huku kazi zisizohitaji ujuzi wakipewa vijana wa kata mradi utapopita.
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Julieth Payovela, ameyabainisha hayo leo, wakati wa hafla fupi ya kukabidhii mabomba kwa mkandarasi kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, umeshafikia asilimia tatu ya utekelezaji wake.
Amesema, mradi unatekelezwa ndani ya miezi 24 na utakapokamilika utahudumia wakazi 189,936 kutoka kata 11 na vijiji 54 kati ya 20 na vijiji 58 na utakuwa umeongeza asilimia 85 ya upatikanaji wa maji katika halmashauri hiyo.
Amezitaja kata hizo kuwa ni Igunda, Kisuke, kinamapula, Nyamilangano, Mapamba, uyogo, Bukomela, Ukune, Mpunze, Ushetu na Ulowa, utasaidia kupunguza magonjwa ya mlipuko ya kuhara, kipundupindu na homa ya matumbo.
Mkazi wa Ulowa, Tihan Stephen, amesema wanatumia maji ya kwenye visima ambavyo wamechimba kwenye makazi yao na wamekuwa wakiugua homa ya matumba mara kwa mara hasa watoto na kuiomba serikali kumsisitiza mkandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji wake, ili ukamilike na waondokane na magonjwa hayo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED